
Kiongozi wa zamani wa Chama cha Leba nchini Uingereza Jeremy Corbyn amesema, waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Tony Blair sio tu hafai kupewa mamlaka ya uliwali wa kuendesha eneo la Ukanda wa Ghaza, lakini hastahili kuwepo popote katika Mashariki ya Kati.
Corbyn ameeleza hayo katika ujumbele alioweka kwenye mtandao wa kijamii wa X akisema: “uamuzi wa kimajanga aliochukua Tony Blair wa kuivamia Iraq uligharimu maelfu kwa maelfu ya maisha. Hapasi kuwapo popote karibu na Mashariki ya Kati, achilia mbali Ghaza. Si juu ya Blair, Trump au Netanyahu kuamua mustakabali wa Ghaza. Hilo ni juu ya watu wa Palestina.”
Kiongozi huyo wa zamani wa chama cha Leba nchini Uingereza amesisitiza juu ya hayo kufuatia matamshi yaliyotolewa na rais wa Marekani Donald Trump kwamba Blair amepangwa kuwa sehemu ya uongozi utakaokuwa na mamlaka ya uendeshaji wa eneo Ghaza katika kipindi cha mpito cha baada ya vita vya mauaji ya kimbari yanayoendelezwa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya eneo hilo.
Kabla ya hapo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ilitoa msimamo wake juu ya suala hilo kwa kutangaza kuwa, watu wa Palestina wanao uwezo wa kusimamia mambo yao wenyewe.
Kupitia mjumbe wake wa ofisi ya kisiasa Husam Badran, Hamas imemtaja Blair kuwa ni ‘ndugu wa shetani’ na kusisitiza kuwa, badala ya waziri mkuu huyo wa zamani wa Uingereza kufanywa gavana wa muda wa Gaza, “[anastahili] kusimamishwa mbele ya mahakama za kimataifa kwa uhalifu wake, hasa nafasi yake katika vita vya Iraq (2003-2011).”
Badran amemuelezea zaidi Blair kuwa ni mtu ambaye “hajaleta lolote jema kwa piganio tukufu la Palestina, Waarabu au Waislamu, akibainisha kwamba “nafasi yake ya uhalifu, uharibifu imekuwa ikijulikana kwa miaka mingi.”
Amesisitiza kuwa, kusimamia masuala ya Wapalestina huko Ghaza au Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni suala linaloihusu Palestina tu na linapasa liamuliwe kwa makubaliano ya kitaifa na si kuamriwa na wadau wa kikanda au kimataifa…/