“Tukiangalia misukosuko haimo peke yake kwenye jumuiya, iko kila mahali duniani pote, lakini hatuna hofu,” amesema Nduva. Akiiongeza kwamba EAC inashirikiana na Jumuiya yamaendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC, Umoja wa Afrika na hata Marekani katika kuhakikisha utulivu unadumishwa.
Bi. Nduva ameleza juhudi za kanda hiyo katika kuendeleza mazungumzo ya amani kwa ajili ya maeneo yenye migogoro, ikiwemo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Sudan Kusini, Rwanda, Burundi na Somalia. “Tumefanikisha uteuzi wa viongozi wa mazungumzo hayo, wakiwemo wanawake wawili, ambao watasaidia kupata suluhisho la kudumu,” amesema Nduva.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, Veronica Nduva, akizungumza na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kandoni mwa Mjadala Mkuu wa UNGA80 jijini New York Marekani.
Kuzidisha uwekezaji na uchumi endelevu
Nduva pia amefafanua juu ya changamoto za kifedha zinazokumba kanda hiyo kutokana na upungufu wa ufadhili wa kimataifa.
“Tumezungumza kwa kina na muhimu ni kuchukua pesa kidogo tulizo nazo na kuziweka kwenye miradi yenye matokeo chanya,” amesema. Amesisitiza kuwa EAC inalenga kuhakikisha maendeleo endelevu yanapatikana hata wakati ufadhili wa nje unapungua.
Aidha, Nduva amebainisha mafanikio ya kanda katika kuboresha masuala ya kidijitali, ikiwemo kuweka mifumo ya malipo ya kidijitali kati ya mipaka ya nchi wanachama.
“Hii ni mbinu moja ambayo tumeleta maendeleo kwenye uchuuzi na kujiendeleza kwa wananchi wa jumuiya,” amesema.
Demokrasia na uchaguzi wa amani
Kuhusu uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu katika baadhi ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bi. Nduva amesema jumuiya inaangalia masuala ya demokrasia, amani na usalama kwa ukaribu.
Amesema “Tunahamasisha demokrasia yetu na ninaamini yote yatakuwa sawa. Kwa Tanzania, tunaweza pia huenda kukashuhudiwa historia ya mama wa kwanza kuchaguliwa rasmi kidemokrasia.”
Maendeleo ya kimataifa na masuala ya kidijitali
Nduva pia ameelezea uzoefu wake kutoka kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa ulioadhimisha mwaka wa themanini.
“Mijadala ni ya kusisimua sana nimefurahia kuona msisitizo wa kutumia teknolojia ya kidijitali, ikiwemo Akili Mnemba AI, katika kuweka miundo msingi ya maendeleo,” amesema.
Katibu Mkuu huyo wa EAC amemalizia mahojiano yake na Idhaa ya Kiswahili kwa kusema kuwa, licha ya changamoto za kifedha na kisiasa, jumuiya inaendelea kuweka vipaumbele vinavyolenga maendeleo endelevu, usalama na demokrasia katika ukanda wa Afrika Mashariki.