
Rais wa Marekani ambaye ndiye chanzo kikuu cha mauaji ya umati huko Ghaza kwa uungaji mkono wake wa hali ya juu kwa utawala wa Kizayuni, kwa mara nyingine tena amejifanya eti anataka kukomeshwa vita Ghaza, sambamba na kuiunga mkono kikamilifu Israel. HAMAS imepinga mpango huo ikisisitiza kuwa hauna jipya na hauna dhamana yoyote ya kutekelezwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Mahmoud Mardawi, kiongozi wa harakati ya Hamas ya Palestina alisisitiza jana Jumatatu kwamba mpango unaodaiwa ni wa Trump wa eti kukomesha vita Ghaza, kwanza haujaifikia Hamas au chama kingine chochote cha Palestina lakini kwa jinsi alivyopata tetesi zake, mpango huo hauna maana.
Amedokeza kwamba hana ufahamu wa kina kuhusu mpango huo, lakini mpango wowote usiolinda haki za Wapalestina, haukubaliwi na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS.
Kuhusu madai ya Trump ya kuupokonya silaha Muqawama wa Palestina, Mardawi amesema: “Silaha za Muqawama hazijamdhuru Mpalestina yeyote wala nchi jirani hadi sasa. Lengo pekee la silaha hizo ni kupambana na utawala wa Kizayuni na kukomboa ardhi za Palestina.
Rais wa Marekani, Donald Trump alisema mbele ya waandishi wa habari akiwa pamoja na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwamba eti amekaribia sana kutatua mgogoro wa Palestina na kudai kwamba eti mpango mpya wa amani wa Washington haubuniwa tu kusimamisha vita huko Ghaza lakini pia kuweka amani ya kudumu katika Mashariki ya Kati.
Vilevile Mardawi amesema kwamba HAMAS inaamini kuwa lengo la mpango huo wa Trump na hatua za hivi karibuni za Marekani ni kujaribu kudhoofisha tu harakati za kimataifa za kulitambua taifa huru la Palestina.
Pia amesema: “Kamwe Hamas haitakubali pendekezo lolote ambalo halijumuishi haki ya wananchi wa Palestina ya kujiamulia wenyewe hatima yao na kuwapa kinga ya kutoshambuliwa.”