Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ameikosoa Marekani na mataifa matatu ya Ulaya kwa kujaribu kutumia utaratibu wa ‘snapback’ wa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 ili kurejesha tena vikwazo vilivyokwisha muda wake vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Araghchi ametangaza msimamo huo katika mazungumzo aliyofanya na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ambapo alikuelezea kurejeshwa tena kwa vikwazo kuwa ni “pigo kubwa kwa diplomasia” na dalili ya kutokuwa na nia njema mataifa husika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani vitendo vya Marekani na madola ya Ulaya akisema “havihalalishiki na ni kinyume cha kisheria.”

Amesisitiza kuwa vikwazo vyote dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, ulioanzishwa chini ya azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, vinatarajiwa kumalizika tarehe 18 Oktoba.

Mnamo tarehe 19 Septemba, Baraza la Usalama lenye wanachama 15 lilishindwa kupitisha azimio ambalo lingezuia kuwekwa tena vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran baada ya nchi tatu za Ulaya zinazounda Troika ya nchi za bara hilo E3 Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuanzisha utaratibu wa “snapback” na kuituhumu Tehran kuwa eti imeshindwa kutekeleza kikamilifu Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA).

Azimio la pili lililopendekezwa na Russia na China linalofanana na hilo, ambalo lilitaka kuongezewa muda wa miezi sita JCPOA na azimio nambari 2231, nalo pia lilishindwa kupitishwa katika Baraza la Usalama siku ya Ijumaa iliyopita.

Baraza la Usalama la UN lilirejesha vikwazo hivyo jana Jumapili Septemba 29. Kufuatia hatua hiyo mali za Iran nje ya nchi zitazuiliwa tena, mikataba ya silaha iliyosaini na nchi zingine itasimamishwa na kulenga mpango wake wa makombora ya ulinzi utawekewa vikwazo.

Mwezi uliopita, E3 ilitumia kinachojulikana kama utaratibu wa snapback, mchakato wa siku 30 kurejesha vikwazo vyote dhidi ya Iran.

Iran ilipinga hatua hiyo na kusema kuwa ni kinyume cha sheria, ikitolea mfano hatua ya Marekani ya kujitoa katika mapatano ya JCPOA na uamuzi wa nchi hizo tatu za Ulaya wa kufungamana na vikwazo vilivyo kinyume cha sheria vilivyowekwa na Washington dhidi ya Iran baada ya hatua hiyo badala ya kutekeleza majukumu yao ya JCPOA…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *