Wananchi wa Afrika Kusini walifanya maandamano makubwa na ya kihistoria hivi karibuni wakitaka kuvunjwa kikamilifu uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara wa nchi hiyo na utawala dhalimu na wa ubaguzi wa rangi wa Israel.
Zaidi ya wanaharakati elfu tatu, mashirika yasiyo ya kiserikali na vyama vya kisiasa vya Afrika Kusini walifanya maandamano katika mitaa ya mji wa Cape Town, wakiitaka serikali ya nchi hiyo kuvunja uhusiano wake wa kibiashara na kidiplomasia na Israel kutokana na vita vya Ghaza na kufunga ubalozi wa utawala huo mjini Pretoria.
Maandamano hayo ambayo ni miongoni mwa maandamano makubwa zaidi ya kuunga mkono Palestina nchini Afrika Kusini yanaakisi mashinikizo yanayozidi kuongezeka duniani hususan kutoka nchi za Afrika dhidi ya utawala wa Kizayuni wa kutaka kukomeshwa vita huko Ghaza.
Afrika Kusini, nchi yenye historia ya kupambana na ubaguzi wa rangi sasa iko mstari wa mbele katika kukosoa sera za kikatili za Israel. Kumbukumbu ya vikwazo vya kimataifa dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini imekuwa kielelezo cha kukabiliana na ukiukaji wa haki za binadamu huko Palestina. Wanaharakati na maafisa wengi wa Afrika Kusini wanaamini kwamba ulimwengu unapaswa kukabiliana na sera za kibaguzi za Israel kama ilivyokabiliana na ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini. Mlingano huu wa kihistoria haufai tu kutumika kwa ajili ya kuonesha maadili na haki za binadamu, bali unapaswa kutumika pia kuimarisha uhalali wa kuchukuliwa hatua za kuuwekea vikwazo utawala wa Kizayuni.

Kwa upande wake, mmoja wa Waratibu wa Kampeni ya Mshikamano wa Palestina, alitumia fursa ya maandamano hayo kutoa mwito wa kuchukuliwa hatua za kivitendo na serikali ya Afrika Kusini, ikiwa ni pamoja na kumfukuza balozi wa Israel, kufunga ubalozi wa utawala huo mjini Pretoria, kusimamisha mauzo ya makaa ya mawe na kuiondoa Israel katika taasisi za kimataifa za michezo. Jambo hilo linaonesha kubadilika mbinu za mapambano dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni, kimataifa. Mratibu huyo alikumbushia tajriba na uzoefu wa vikwazo vya kimataifa dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini akisisitiza kuwa, sasa ni wakati wa Afrika Kusini kuchukua msimamo kama huo dhidi ya Israel.
Hali ya kibinadamu huko Ghaza ni mbaya sana. Israel inaendelea kupuuza maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ya kuitaka ikomeshe jinai zake huko Ghaza. Ripoti zinaonyesha kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi tangu kuanza vita vya Ghaza imeshapindukia 66,000; huku utawala wa Kizayuni ukitangaza nia ya kuendeleza mashambulizi yake dhidi ya Ghaza hadi utakapoikalia kwa mabavu kikamilifu. Takwimu hizi za kushtua hazioneshi tu ukubwa wa maafa ya kibinadamu huko Ghaza, bali pia zinaonyesha kuwa Israel, licha ya kulaaniwa kimataifa, inaendelea kutenda jinai za kuchupa mipaka dhidi ya Wapalestina.
Lakini wimbi la kulaaniwa jinai za Israel kimataifa linazidi kuwa kubwa. Nchi za Afrika ambazo zenyewe zimekuwa wahanga wa ukoloni na ubaguzi wa rangi, sasa hivi zinailaani Israel na kusema ni utawala wa kibaguzi, na baadhi ya nchi hizo pia zimekatisha kivitendo uhusiano wao wa kidiplomasia na kiuchumi na Israel.
Katika upande mwingine, vikwazo vya kiuchumi vya raia na wananchi wa mataifa ya dunia dhidi ya utawala wa Kizayuni navyo vinazidi kuwa vikubwa. Makampuni kama vile Starbucks na McDonald’s ambayo yanashirikiana moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na Israel, yamekumbwa na vikwazo vya walimwengu na kupelekea kushuka kwa kasi mauzo kiasi kwamba yamelazimika kufunga baadhi ya matawi. Starbucks imetangaza kuwa imelazimika kufuta nafasi elfu moja za kazi katika matawi yake ya nchini Marekani na Uingereza na kufunga baadhi ya matawi yake yaliyopata hasara kutokana na vikwazo vya walimwengu. Kampuni ya Marekani ya McDonald’s, ambayo ilitoa chakula cha bure kwa wanajeshi wa Israel katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, pia imekiri kwamba vita vya Ghaza na vikwazo vya walimwengu dhidi ya kampuni hiyo vimekuwa na taathira hasi katika mauzo yake.
Kwa jumla, mashinikizo ya kimataifa, maandamano makubwa ya kila kona sambamba na hatua za kidiplomasia na vikwazo vya kiuchumi, yote hayo yanaonesha kushadidi mno upinzani dhidi ya Israel duniani.
Uzoefu wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini umeonesha kuwa mashinikizo makubwa ya kiutamaduni na kimataifa yanaweza kuwapigisha magoti Wazayuni. Ingawa njia ya kuisusia Israel bado inakabiliwa na vikwazo vingi, lakini wimbi la maandamano ya kimataifa na kuongezeka mwamko wa walimwengu wa kuiunga mkono Palestina ni mambo ambayo yanazidi kuthibitisha kwamba kama ilivyokuwa wakati wa kukata roho utawala wa makaburu huko Afrika Kusini, hivi sasa pia utawala katili wa Kizayuni unakabiliwa na hatima ile ile ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini.