Leo ni Jumanne tarehe 7 Rabiul-Thani mwaka 1447 Hijria Qamaria, sawa na tarehe 8 mwezi Mehr mwaka 1404 Hijria Shamsia inayosadifiana na tarehe 30 Septemba 2025 Miladia.
Siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, yaani tarehe 8 Mehr, ni maarufu hapa nchini Iran kama siku ya kumuenzi Maulana Jalaluddin Muhammad bin Bahauddin maarufu kwa jina la Moulavi. Maulana Jalaluddin alizaliwa mwaka 604 Hijria Qamaria katika mji wa Balkh uliokuwa moja kati ya miji ya Iran ya kipindi hicho. Moulavi alikuwa gwiji wa mashairi na malenga mwenye uwezo na kipaji kikubwa katika karne ya 7 Hijria. Miongoni mwa athari kubwa za Maulana au Jalaluddin Balkhi ni kitabu cha mashairi cha Masnavi Maanavi.

Miaka 87 iliyopita katika siku kama ya leo ulifayika mkutano wa kihistoria wa Munich nchini Ujerumani. Mkutano huo ulihudhuriwa na Adolph Hitler na Benito Mussolini viongozi wa Ujerumani na Italia na pia Neville Chamberlain na Edouard Daladier, Mawaziri Wakuu wa wakati huo wa Ufaransa na Uingereza. Mkutano huo wa Munich ulifanyika kwa shabaha ya kutafuta njia ya kumaliza hitilafu kati ya Ujerumani na Czechoslovakia. Mkutano huo ulimalizika kwa kufikiwa makubaliano ya kuiunganisha sehemu moja ya ardhi ya Czechoslovakia na Ujerumani.

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita yaani tarehe 30 mwezi Septemba mwaka 1966, nchi ya Botswana ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Botswana ilianza kukoloniwa na Uingereza mwaka 1885 Miladia. Harakati za wananchi wa Botswana za kuikomboa nchi yao zilishtadi tangu mwaka 1920 na kupelekea kupatikana uhuru wa nchi hiyo mwaka 1966. Nchi ya Bostwana iko kusini mwa bara la Afrika ikipakana na Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia.
Na Miaka 40 iliyopita, alifariki dunia mvumbuzi wa kipimo kinachotumiwa kupimia nguvu ya mtetemeko wa ardhi Charles Richter. Akishirikiana na mhakiki mwingine, Richter alipima mtetemeko huo kwa mujibu wa nishati inayotokana na mawimbi ya mitetemeko ya ardhi toka daraja moja hadi 9 na kusajili kipimo cha Rishta. Kabla ya hapo wataalamu walikuwa wakipima mitetemeko ya ardhi kwa kutegemea athari ya nje ya kipimo ambacho hakikuwa cha kuaminika.
