
Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesisitiza kwamba, mpango wa Donald Trump kwa ajili ya Ukanda wa Ghaza ni mpango wa utawala wa Kizayuni na ni waraka wa agizo la kuendeleza uchokozi na uvamizi dhidi ya wananchi wa Palestina.
Ziad al-Nakhalah amesema, kilichotangazwa katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya rais wa Marekani Donald Trump na waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ni makubaliano ya Washington na Tel Aviv na ni kauli inayoakisi matakwa ya utawala wa kizayuni.
Al-Nakhlah ameongezea kwa kusema: “huu ni waraka wa agizo la kuendeleza uchokozi dhidi ya watu wa Palestina; na Israel inajaribu kupata kupitia Marekani kile ambacho haijaweza kukipata kupitia vita”.
Katibu Mkuu wa Jihadul-Islami amebainisha kwa kusema: “sisi tunauchukulia mpango huu wa Marekani na Israel kama hati za kuliingiza eneo kwenye hali ya mripuko”.
Wakati huohuo, Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen ametangaza kuwa mpango wa Donald Trump kwa ajili ya Ghaza hautekelezeki.
Mohammed al-Farah, amesema: “mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani hautekelezeki na lengo lake ni kuitupa nje ya ulingo Hamas na kuifanya ionekane kuwa ndiyo inayobeba dhima ya vita”.
Ameongeza kuwa, mpango huo wa Trump unalenga kupunguza hasira za walimwengu dhidi ya Israel na kufuta mshikamano wa ulimwengu na Palestina.
Jana Jumatatu, Rais wa Marekani, Donald Trump alitamka mbele ya waandishi wa habari akiwa pamoja na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwamba eti amekaribia sana kutatua mgogoro wa Palestina na kudai kuwa kile alichokiita mpango mpya wa amani wa Washington haujabuniwa kusimamisha vita tu huko Ghaza lakini pia kujenga amani ya kudumu katika Mashariki ya Kati…/