Akihutubia Baraza la Usalama jijini New York, Marekani leo lililokutana kupata ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu hali Mashariki ya taifa hilo la Maziwa Makuu, Bi. Keita ametoa tathmini ya kuongezeka kwa ghasia, kusimama kwa mchakato wa kisiasa, na kuzorota kwa hali ya kibinadamu, huku akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kuziba pengo kati ya ahadi na hali halisi.

“Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bado ni ahadi zaidi ya uhalisia,” Bi. Keita ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, DRC, MONUSCO, amewaambia wajumbe wa Baraza.

“Kuna tofauti kubwa kati ya maendeleo tunayoyaona kwa maandishi na uhalisia tulioko nao mashinani, ambako kunaendelea kutawaliwa na vurugu.”

Kuongezeka kwa ghasia licha ya juhudi za kidiplomasia

Keita ametambua mafanikio kadhaa ya kidiplomasia tangu kutiwa saini kwa Mkataba wa Washington tarehe 27 Juni, ikiwa ni pamoja na kurejelewa kwa mazungumzo ya amani, upatanishi wa kikanda, na ushiriki mkubwa zaidi kutoka kwa taasisi za kikanda kama Muungano wa Afrika, (AU),  Jumuiya ya Afrika Mashariki. (EAC), na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Tamko la kanuni za msingi lilitiwa saini kati ya serikali ya DRC na kundi la M23/AFC mwezi Julai, na mazungumzo yakaendelea Doha, Qatar.

Hata hivyo, amesema maendeleo haya hayajabadilisha hali ya usalama. MONUSCO imerekodi vifo vya raia zaidi ya 1,000 jimboni  Ituri na Kivu Kaskazini tangu mwezi Juni pekee. Mwezi Julai ulikuwa na vifo vingi zaidi katika wilaya ya Rutshuru tangu M23 iliporejea kwa nguvu mwaka 2021.

Keita amesisitiza kuendelea kwa upanuzi wa M23/AFC katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, kupuuza Azimio la Baraza la Usalama Na. 2773, na kuanzisha utawala sambamba, jambo linalodhoofisha taasisi za serikali na kuchochea ukosefu wa usalama. “Takribani watu 7,000 wameripotiwa kujiunga na kundi hilo tangu mwezi Februari,” amesema Bi. Keita.

“Baada ya miezi minane, vipengele muhimu vya Azimio 2773 bado havijatekelezwa,” amesema Keita, akitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano bila masharti yoyote na kufikiwa kwa makubaliano ya amani ya kudumu.

Walinda amani wa Indonesia kutoka MONUSCO wanashika doria karibu na Bunia.

MONUSCO/Didier Vignon Dossou-Gba

Walinda amani wa Indonesia kutoka MONUSCO wanashika doria karibu na Bunia.

Mmakundi mengine ya kijeshi yachochea machafuko

Mbali na M23/AFC, makundi mengine yenye silaha yanaendelea kuwatisha raia. Waasi wa ADF wanaohusishwa na magaidi wa ISIS wamewaua angalau raia 300 katika miezi mitatu iliyopita, mara nyingi wakilenga ibada za kidini na mazishi.

Jimboni Ituri, mapigano kati ya jeshi la DRC (FARDC)  na kikundi cha CRP, pamoja na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka waasi wa CODECO, yamesababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao. MONUSCO iliwahifadhi raia 3,500 katika kituo chake cha Gina kufuatia mapigano hayo.

Keita amehimiza makundi yenye silaha yanayoshiriki katika mazungumzo ya amani ya Aru II kutimiza ahadi zao, ikiwa ni pamoja na kuwaachilia watoto 400 wanaowashikilia.

Haki za binadamu na mgogoro wa kibinadamu wazidi kuzorota

Hali ya haki za binadamu nayo inazidi kuwa mbaya, hasa huko Kivu Kusini, ambayo haiko tena chini ya mamlaka ya moja kwa moja ya MONUSCO tangu Julai 2024. Makundi kama Wazalendo yanaendelea kutekeleza ukiukaji mkubwa wa haki, ikiwa ni pamoja na ubakaji unaohusiana na vita.

Vizuizi vya M23/AFC kuhusu harakati na upatikanaji wa maeneo vimepunguza sana uwezo wa MONUSCO kuchunguza ukiukaji wa haki. Keita alitoa wito kwa kutumwa mara moja kwa tume huru ya uchunguzi, ambayo bado haijapata ufadhili.

Mlipuko wa Ebola Kasai

Janga la kibinadamu pia limeongezeka kwa kasi. Taifa linakumbwa na mlipuko mpya wa Ebola katika jimbo la Kasai, huku watu milioni 27.7 wakikabiliwa na uhaba wa chakula. Mpango wa Usaidizi kwa DRC uliotangazwa na Umoja wa Mataifa umefadhiliwa kwa asilimia 15.2 tu, ikilinganishwa na asilimia 41 mwaka jana.

“Pengo kati ya mahitaji ya msingi na rasilimali zilizopo linazidi kuwa kubwa,” amesema Keita. “Katika maeneo mengine, msaada umesitishwa. Kwingineko, mgao wa chakula unapunguzwa. Vifo vya akina mama wakati wa kujifungua vinaongezeka.”

Kaskazini Mashariki mwa Kivu, DRC: Tarehe 3 Desemba 2024, kikosi cha Morocco cha Munigi POB kilifanya doria katika kambi ya Kanyaruchinya kwa ajili ya watu waliokimbia makazi. Lengo la mpango huu lilikuwa kuimarisha usalama na kuhakikisha ulinzi wa raia …

MONUSCO/Aubin Mukoni

Uwezo wa MONUSCO wazidi kudhoofika

Keita pia ameonya kwamba uwezo wa MONUSCO kuwalinda raia unazidi kudhoofishwa na uhaba wa mafuta, ucheleweshaji wa usambazaji wa chakula, mzunguko wa askari uliokwama, na vikwazo vya upatikanaji wa miundombinu, hasa karibu na Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, ambako uwanja wa ndege bado umefungwa.

“Bila hali hizi kurekebishwa, MONUSCO haiwezi kutekeleza kikamilifu jukumu la ulinzi lililopewa na Baraza hili,” amesema.

Licha ya changamoto hizo, MONUSCO inaendelea kuwahifadhi raia, kuondoa mabomu yaliyosalia ardhini, na kuunga mkono uwajibikaji wa kisheria. Ujumbe huo pia umewasaidia takribani waathiriwa 400 wa ubakaji unaohusiana na vita mwaka huu, na kusaidia kuwarejesha makwao wapiganaji wa zamani pamoja na kuwarudisha kwenye jamii.

Mapendekezo na wito wa dharura

Katika hitimisho lake, Keita ametoa mapendekezo makuu kwa Baraza la Usalama na jumuiya ya kimataifa:

  1. Kusisitiza usitishaji wa mapigano wa kudumu na kufanikisha makubaliano ya amani ya kweli.
  2. Kuhakikisha utekelezaji kamili wa Azimio 2773, hasa kuondolewa kwa M23/AFC kutoka maeneo waliyochukua.
  3. Kurejesha uwezo kamili wa operesheni za MONUSCO, ikiwa ni pamoja na mzunguko wa askari na upatikanaji wa miundombinu muhimu.
  4. Kutuma tume huru ya uchunguzi kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu.
  5. Kufunga pengo la ufadhili kwa misaada ya kibinadamu, hasa wakati mahitaji yanaongezeka.
  6. Kukabiliana na sababu kuu za migogoro, ikiwa ni pamoja na uchimbaji haramu wa madini, uporaji wa rasilimali, na mtiririko haramu wa fedha.
Watu wakimbia makazi yao huku mapigano yakiendelea kati ya FARDC na waasi wa M23 katika eneo la Rutshuru.

UN Photo/S. Liechti

Keita pia amesisitiza jukumu muhimu la wanawake wa DRC katika ujenzi wa amani, na kutoa wito kwa ushiriki wao kikamilifu katika mchakato mzima, akitambua kumbukumbu ya miaka 25 ya Azimio la Baraza la Usalama la UN  namba 1325 kuhusu wanawake, amani na usalama.

Amekumbusha kuwa “kuziba mapengo haya si hiari,” Keita amehitimisha akiongeza kuwa, “ni njia pekee ya kulinda maisha na kuipa amani nafasi. Maazimio yatakuwa na maana tu iwapo yataambatana na hatua halisi mashinani. Tukishindwa kuziba pengo hili, mamilioni ya raia wataendelea kulipa gharama.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *