Indileni Daniel Waziri wa Mazingira, Misitu na Utalii wa Namibia amesema kuwa nchi yake imeathiriwa na moto mkubwa wa nyika ambao umeteketeza zaidi ya theluthi moja ya Mbuga ya Taifa ya Etosha, mojawapo ya hifadhi kubwa zaidi barani Afrika.

Akizungumza jana usiku na Shirika la Utangazaji la Namibia (NBC), Waziri wa Mazingira, Misitu na Utalii wa nchi hiyo amebainisha kuwa: “Moto mwingi umedhibitiwa, hakukuwa na moto unaoonekana tulipokuwa angani ingawa timu bado zinafanya kazi ya kuzima maeneo madogo ambayo yanaendelea kuwaka,” 

Amesema, wazima moto wataendelea kupiga doria mbugani ili kuzuia kuibuka tena moto. 

Moto ulianza kuwaka katika mbuga ya taifa ya Namibia ya Etosha tarehe 22 mwezi huu wa Septemba na kuenea haraka katika mbuga hiyo huku dalili zikionyesha kuwa kulikuwa na shughuli za uchomaji mkaa katika mashamba jirani na mbuga hiyo. 

Kiwango cha uharibifu na hasara bado hakijafahamika lakini ripoti za awali zinaonyesha kuwa swala tisa wamepoteza maisha katika mbuga hiyo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 22,270. Mbuga ya Taifa ya Namibia pia ni makazi ya  spishi 114 za mamalia, wakiwemo vifaru weusi walio hatarini kutoweka.

Serikali ya Namibia siku ya Jumapili ilituma askari 500 katika mbuga hiyo kusaidia zoezi la uzimaji moto. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *