
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja utaratibu wa Snapback kama jaribio la kuhalalisha vitendo haramu vya nchi za Magharibi.
Rais Pezeshkian amebainisha masuala mbalimbali na kuhusu sera na stratejia za Iran katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya al Arabi.
Rais wa Iran amesema kuwa makubaliano ya Cairo kwa mara nyingine tena yamedhihirisha uaminifu wa Iran na unafiki wa Marekani na Ulaya katika kadhia ya nyuklia na kusisitiza kuwa: “Ninaamini kwamba kwa ushirikiano, maelewano na umoja ambao umejengeka ndani ya nchi, na vilevile kwa mafungamano tuliyo nayo na majirani zetu na nchi nyingine duniani tutaweza kutatua matatizo yetu.”
Rais Pezeshkian amesisitiza umuhimu wa kubainisha wazi msimamo wa Iran kwa jamii ya kimataifa. Aidha amekosoa hatua ya Baraza la Usalama ya kupasisha utaratibu wa Snapback akisisitiza kuwa baraza hilo halifuati sheria bali mashininikizo ya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya.
Huku akieleza wazi unafiki wa nchi zinazoituhumu Iran eti haijaheshimu makubaliano ya JCPOA, Rais wa Iran amesema na hapa ninamnukuu: “Tulifungamana na makubalino tuliyo saini lakini Marekani ndiyo iliyokiuka makubaliano hayo kwa kujiondoa katika makubaliano hayo.
Rais Masoud Pezeshkian pia amezungumzia makubaliano ya hivi karibuni yailyofikiwa kati ya Iran na IAEA kupitia upatanishi wa Misri. Amesema, makubaliano hayo yameanzisha mfumo wa ushirikiano na kwamba tehran imetangaza kuwa tayari kushirikiana na wakala wa IAEA.