
Russsia imesema kuwa jeshi lake linachunguza iwapo Marekani itaikabidhi Ukraine makombora ya meli ya Tomahawk au la kwa ajili ya kutekeleza mashambulizi dhidi yake; hatua ambayo maafisa wa Russia wanasema inaweza kusababisha mzozo mkubwa.
JD Vance Makamu wa Rais wa Marekani alisema siku ya Jumapili kwamba Washington inapitia ombi la Ukraine kwa ajili ya kupatiwa makombora ya Tomahawk.
Rais Donald Trump hadi sasa bado hajachukua uamuzi wa mwisho, na amekuwa akitiwa wasiwasi na kushtadi mzozo wa Ukraine na kutumbukia katika makabiliano ya moja kwa moja na Russia.
Russia Jumatatu wiki hii ilisema kuwa jeshi lake linachunguza iwapo Marekani itaitumia Ukraine makombora ya Tomahawk au la kwa lengo la kutekeleza mashambulizi katika ardhi ya Russia.
Rais Vladimir Putin wa Russia aliwahi kusema huko nyuma kuwa Russia ina haki ya kushambulia taasisi za kijeshi katika nchi ambazo zinaoiruhusu Ukraine kutumia makombora yao kuipiga Russia.
Andrei Kartapolov Mkuu wa Kamati ya Ulinzi katika Bunge la Russia amesema wataalamu wowote wa kijeshi wa Marekani waliisaidia Ukraine kurusha makombora ya Tomahawk dhidi ya Russia watakuwa shabaha ya Moscow. “Hakuna mtu atakayewalinda. Si Trump, si Kellogg, wala mtu mwingine yeyote,” amesema Mkuu wa Kamati ya Ulinzi katika Bunge la Russia.
Keith Kellogg Mjumbe Maalumu wa Marekani nchini Ukraine amesema kuwa Trump ameeleza kuwa Kyiv inapasa sasa kuwa na uwezo wa kufanya mashambulizi ya masafa marefu dhidi ya Russia.