
Iran imetangaza leo Jumanne, Septemba 30, kurejea wiki hii kwa raia wake 120 waliofukuzwa nchini Marekani, kama sehemu ya sera ya Rais Donald Trump ya kupinga uhamiaji. Uamuzi huu, mfano adimu wa ushirikiano kati ya Washington na Tehran, unakuja baada ya miezi kadhaa ya majadiliano, kulingana na gazeti la New York Times.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Watu 120 wanatarajiwa kufukuzwa na kurejea nchini katika siku mbili zijazo,” Hossein Noushabadi, afisa wa masuala ya kibalozi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ameliambia shirika la habari la Tasnim. “Mamlaka ya uhamiaji ya Marekani imeamua kuwatimua takriban Wairan 400 waliopo Marekani kwa sasa, wengi wao waliingia kinyume cha sheria,” ameongeza.
Gazeti la New York Times, likiwanukuu maafisa wawili wa Iran na Mmarekani mmoja ambaye hakutaka kutajwa majina, limeripoti Jumanne kwamba takriban wakimbizi 100 wa Iran nchini Marekani wamerudishwa nchini mwao kufuatia makubaliano kati ya Washington na Tehran. Ikiwasiliana na shirika la habari la AFP, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani bado haijajibu ombi la kutoa maoni.
Mawasiliano yamefanyika kati ya Tehran na Washington ili kuwezesha kurejea kwa raia wa Iran. “Tumeomba kwamba haki za kiraia za raia wetu ziheshimiwe,” waziri wa mambo ya nje wa Iran amesema. Iran “imetuma maelezo kwa upande wa Marekani kupitia Ofisi ya Kulinda Maslahi ya Iran nchini Marekani” na “inafuatilia hali hiyo,” Hossein Noushabadi amesema, akinukuliwa na Tasnim.
Uhamisho wenye utata
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, raia 120 wa Iran waliofukuzwa kutoka Marekani watarejea nchini kwa ndege ya kukodi kupitia Qatar, anaripoti mwandishi wetu mjini Tehran, Siavosh Ghazi. Ndege iliyokodishwa na mamlaka ya Marekani ilipaa kutoka Louisiana siku ya Jumatatu jioni na inatarajiwa kutua Iran baadaye Jumanne, linaripoti Gazeti la New York Times.
Uhamisho huu unajumuisha “jaribio la wazi zaidi hadi sasa la utawala wa Trump kuwafukuza wahamiaji bila kuzingatia hali kuhusiana na haki za binadamu wanazoweza kukabiliana nazo,” gazeti hilo linaongeza.
Mapema mwaka huu, Marekani iliwafukuza wakimbizi wa Iran, wengi wao Wakristo, hadi Costa Rica na Panama. Mamilioni kadhaa ya Wairan wanaishi Marekani au wana kadi za kuishi Marekani, lakini hawaishi nchini humo.
Vizuizi hivi vipya vya serikali ya Marekani vinatatiza kusafiri kwa Wairan ambao wana kadi za kuishi nchini humo. Haya yanajiri huku uhusiano kati ya nchi hizo mbili ukizidi kuwa mgumu, hasa kufuatia mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran, lakini pia sera ya shinikizo la juu iliyoamuliwa na serikali ya Rais Trump dhidi ya Iran.