Rais wa Marekani Donald Trump amewashambulia vikali kwa kuwaita wapumbavu washirika wakuu wa Ulaya wa nchi hiyo ikiwemo Uingereza na Ufaransa kwa kuitambua rasmi nchi ya Palestina.

Mataifa kadhaa ya ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ufaransa, Canada, Australia, Ureno, Ubelgiji, Malta, Luxembourg, San Marino na Andorra zilitangaza kuitambua rasmi nchi ya Palestina wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika wiki iliyopita, hatua ambayo ililaaniwa na Marekani na mwitifaki wake mkuu utawala wa kizayuni wa Israel.

Akizungumza jana Jumatatu mbele ya waandishi wa habari katika Ikulu ya White House akiwa pamoja naye waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Trump alisema: “nchi kadhaa zimeitambua ‘kipumbavu’ nchi ya Palestina. Baadhi ya marafiki zetu wa Ulaya, washirika, watu wema”.

Baada ya kuzidunisha na kuzitusi nchi hizo, rais wa Marekani alisema: “lakini kwa kweli, nadhani, wanafanya hivyo kwa sababu wamechoka sana na kile ambacho kimekuwa kikiendelea kwa miongo mingi”.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari uliomalizika bila ya wanahabari kuruhusiwa kuuliza suali lolote, Trump alizindua mpango wake wenye pointi 20 aliouelezea kuwa ni wa kuleta amani, ambao ndani yake unaagiza Harakati ya ukombozi wa Palestina ya Hamas ipokonywe silaha, kuachiliwa mateka wote waliosalia wa Israel kwa mpigo mkabala wa kuachiwa Wapalestina wakiwemo 250 wanaotumikia vifungo vya maisha jela kwenye magereza ya Israel, na kuanzishwa serikali ya mpito huko Ghaza…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *