Leo Jumanne, viongozi wa dunia, maafisa wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia wanakutana New York, Marekani katika mkutano wa ngazi ya juu kukabiliana si tu na dharura ya kibinadamu, bali pia na mkwamo wa kisiasa utokanao na zahma hiyo.
Hatua zitakazochukuliwa katika mkutano huu—sehemu ya wiki ya majadiliano ya ngazi ya juu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa—zina uzito mkubwa, kwani bajeti za misaada zinapungua huku mapigano yakizidi ndani ya Myanmar, na kuwaacha warohingya, moja ya jamii zinazonyanyaswa zaidi duniani wakiwa njia panda.
Wajumbe wanatarajiwa kujadili haki za binadamu na ulinzi wa haki za warohingya ambayo ni kabila dogo, sambamba na jamii nyingine, huku wakitafuta hatua za kisiasa, kijamii na kiusalama kuhakikisha wanarejea nyumbani kwa hiari, kwa usalama na kwa utu.

Hali ya kusubiri isiyoisha
Warohingya, ambao ni kabila dogo na zaidi ya yote waislamu. Kwa muda mrefu wamenyimwa uraia na haki za msingi nchini Myanmar, na walikimbia mashambulizi yaliyofikia kilele mwaka 2017.
Wakati huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN, Zeid Ra’ad al-Hussein, alieleza kitendo hicho kama “mfano halisi wa utokomezaji wa kabila.”
Walipovuka mpaka kuingia Bangladesh, walipata makazi ya dharura katika kile ambacho sasa ni mojawapo ya kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani huko Cox’s Bazar.
Lakini kile kilichoanza kama suluhisho la muda kimegeuka kuwa mgogoro wa kudumu. Wengi wa warohingya hawaoni njia salama ya kurejea Myanmar, ambako utawala wa kijeshi unaendelea kuwanyanyasa wachache na kukabiliana na uasi wa ndani.
Nchini Bangladesh, fursa za elimu na ajira ni finyu, huku matukio ya ukosefu wa usalama, usafirishaji haramu na mvutano na jamii zinazowahifadhi vikiongeza changamoto.
Yunus: Onyo la kusambaratika
Akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa Septemba 26, Mshauri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya Bangladesh, Muhammad Yunus, alitoa onyo kali zaidi kuwahi kutolewa hadi sasa.
“Shirika laUmoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) la Umoja wa Mataifa limeonya juu ya upungufu mkubwa wa fedha. Bila ufadhili mpya wa haraka, mgao wa kila mwezi unaweza kupunguzwa hadi dola 6 tu kwa kila mtu, na kuwaingiza Rohingya kwenye njaa, utapiamlo, na kuwasukuma kuchukua hatua za kukata tamaa,” alisema.
Alitoa wito kwa wafadhili kuongeza msaada wao, lakini alisisitiza kwamba mizizi ya mgogoro iko ndani ya Myanmar:
“Kunyimwa haki na kunyanyaswa kw warohingya, kunakotokana na siasa za utambulisho wa kitamaduni, kunaendelea Rakhine. Mchakato wa kuondoa kutengwa kwa Rohingya hauwezi kucheleweshwa zaidi,” alisema.
“Lazima kuwe na suluhisho la kisiasa linalojumuisha wadau wote ili wawe sehemu ya jamii ya Rakhine wakiwa na haki sawa kama raia kamili.”
Viongozi wengi waliunga mkono hoja hii, wakisisitiza mateso ya warohingya kama kielelezo cha migogoro mikubwa ambayo haijatuliwa kutokana na mkwamo wa kisiasa wa kimataifa.
Guterres: ‘Hatutakata tamaa’
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ambaye alitembelea Cox’s Bazar mapema mwaka huu, alielezea kambi hiyo kama “kumbukumbu ya wazi ya kushindwa kwa dunia kutafuta suluhisho.”
Alisisitiza kuwa suluhisho la msingi ni kurejea kwa hiari, kwa usalama na kwa heshima kwa wakimbizi wa Rohingya nchini Myanmar, na kuwataka wahusika wote kujizuia, kulinda raia na kuunda mazingira ya demokrasia kustawi.
Hata hivyo, mazingira hayo bado hayajafikiwa, hivyo kurudi kwa wakimbizi bado haiwezekani kwa sasa.
Hadi pale mapigano na ukandamizaji wa kimfumo utakapokoma, Guterres alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kutoa msaada kwa wanaohitaji ulinzi nchini Bangladesh.

Mgogoro wa kisiasa wa Myanmar wazidi kuwa mbaya
Baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 1 Februari 2021, Myanmar imetumbukia katika vurugu na hali ya sintofahamu.
Maelfu wameuawa, mamilioni wamekosa makazi na zaidi ya nusu ya watu nchini humo wanahitaji msaada wa kibinadamu. Maafa ya asili kama mafuriko na matetemeko ya ardhi yamezidisha hali mbaya.
Makabila madogo madogo — wakiwemo warohingya,wakachin, washani na wachin — wameathirika vibaya kwa kiasi kikubwa.
Jeshi linatuhumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu kwa kiwango kikubwa, ikiwa ni pamoja na kukamatwa kiholela, mateso na mauaji ya kiholela. Shule, hospitali na nyumba za ibada zimekuwa zikishambuliwa bila kujali.
Tumaini, ujasiri na uvumilivu
Tom Andrews, Mtaalamu Maalum wa UN kuhusu haki za binadamu Myanmar, alisisitiza ujasiri wa watu waliokumbwa na mgogoro huu na hatari kubwa wanazokabiliana nazo.
“Ninaliona katika watu wa Myanmar na ujasiri wao mkubwa. Wananiamsha matumaini. Hawa ndiyo chanzo changu cha tumaini kwamba siku moja jinamizi hili litakwisha,” aliieleza Idhaa ya Umoja wa Mataifa mwaka jana baada ya kuwasilisha ripoti yake kwa Baraza Kuu.
Wakati viongozi wa dunia wakikutana New York, watetezi wa haki wanasema swali kuu si tu kama ufadhili mpya utapatikana, bali kama kuna nia ya kisiasa kumaliza mgogoro huu uliogeuka kuwa ishara ya ukosefu wa mwelekeo na matumaini duniani.