Ofisi za idara ya Udhbiti wa Mafuta na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Nigeria zimefungwa kutokana na mgomo wa kitaifa ulioanzishwa na jumuiya ya wafanyakazi wa sekta ya mafuta baada ya kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote kuwafuta kazi zaidi ya wafanyakazi 800.

Mgomo huo ulioanza jana Jumatatu umeshadidisha mivutano katika nchi hiyo ya Kiafrika mzalishaji mkubwa wa mafuta huku kukiwa na mvutano wa kisheria na kiviwanda ambao unaweza kuvuruga usambazaji wa mafuta na kukwamisha biashara magharibi mwa Afrika khususan kwa nchi zinazotegemea kununua bidhaa za mafuta kutoka Nigeria. 

Jumuiya wa Wafanyakazi Waandamizi wa Petroli na Gesi Asilia ya Nigeria (PENGASSAN) ilisema Ijumaa iliyopita kuwa wafanyakazi katika kiwanda binafsi cha kusafisha mafuta cha Dangote ambacho ni kiwanda kikubwa zaidi barani Afrika walifukuzwa kazi siku ya Alhamisi kufuatia hatua yao ya kutaka kuasisi chama wa wafanyakazi. 

Mgomo huo wa wafanyakazi umesababisha kufungwa ofisi za Tume mbili za Udhibiti wa Petroli za Nigeria. 

Wachambuzi wa mambo kwa upande wao wanahofia kuwa iwapo hali itazidi kuwa mbaya na vyama vingine vya wafanyakazi kujiunga namgomo wa sasa, hatua hiyo inaweza kulemaza shughuli kwenye maeneo ya mafuta, kutatiza utiririshaji wa bidhaa na kusababisha fujo kwenye vituo vya mafuta.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *