
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kurutubisha madini ya urani ni haki isiyopingika na isiyopokonyeka ya Jamhuri ya Kiislamu.
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hayo katika mahojiano na kanali ya CNN yaliyorushwa jana Jumanne na kuongeza kuwa, “Hatujawahi kuwa na hamu yoyote ya kumiliki silaha za nyuklia, na tulithibitisha hili tuliposaini makubaliano ya JCPOA mwaka 2015 na nchi za kundi la 5+1, ikiwemo Marekani.”
Araghchi ameongeza: “Marekani ilishambulia vituo vyetu vya nyuklia na vituo vya urutubishaji urani, na kuviharibu vibaya sana. Hata hivyo, operesheni hiyo ya kijeshi haikuweza kutatua suala hilo kwa sababu teknolojia hiyo ni ya asili na tuna uwezo wa kuifikia na kuipata.”
“Hatukuagiza teknolojia ya nyuklia kutoka nje ya nchi, badala yake, tuliizalisha na kuikuza sisi wenyewe.” Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema na kusisitiza kuwa, “Ni haki yetu kurutubisha urani.”
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amebainisha kuwa, “Hatujawahi kukiuka Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) na daima tumekuwa tukifanya kazi ndani ya mfumo wa sheria za kimataifa.”
Sayyid Araghchi amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haina nia ya kuachana na mpango wake wa nyuklia, ikiwemo kurutubisha madini ya urani, licha ya uvamizi wa kijeshi wa mwezi Juni mwaka huu uliofanywa na Marekani na mutifaki wake wa kieneo, Israel.
Weledi wa mambo wanasisitiza kuwa, hatua ya Iran ya kurutubisha madini ya urani hadi kiwango cha asilimia 60 ni mjibizo kwa vikwazo na mashinikizo ya kimataifa inayowekewa.