
Mahakama ya kijeshi katika Jamhuri yya Kidemokrasia ya Congo imemhukumu adhabu ya kifo aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila, ikimtia hatiani kwa usaliti na uhalifu dhidi ya binadamu.
Hukumu hiyo ilitolewa jana Jumanne na Luteni Jenerali Joseph Mutombo Katalayi, aliyesimamia shauri hilo katika mji mkuu Kinshasa. Jaji huyo alisema kuuwa, Joseph Kabila (54) amepatikana na hatia katika mashtaka yanayojumuisha usaliti, mauaji, unyanyasaji wa kingono, mateso na uasi.
Kabila, ambaye aliongoza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, aliondoka nchini humo mwaka 2023. Hata hivyo, mwezi Mei mwaka huu alionekana kwa muda mfupi katika maeneo ya mashariki ya nchi hiyo yanayodhibitiwa na waasi wa M23.
Kwa sasa haijulikani alipo baada ya hukumu hiyo ya mahakama ya kijeshi.
Kabila alishtakiwa kwa kuunga mkono waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao mwaka huu wametwaa sehemu kubwa ya maeneo ya mashariki yenye utajiri wa madini.
Waendesha mashtaka walisema Kabila alijenga usuhuba na M23 kwa lengo la kuipindua serikali ya Rais Felix Tshisekedi na kurejesha ushawishi wake wa kisiasa.
Kabila, kwa upande wake, amewahi kulaani mashtaka hayo akiyaita “kesi ya maigizo” na kuushutumu mfumo wa mahakama nchini DRC kwa kuwa “chombo cha ukandamizaji”.
Chama chake, People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD), kimesema hukumu hiyo ni uwindwaji wa kisiasa na njama ya kumwondoa mpinzani mkubwa wa serikali.