Tamasha hilo la bia maarufu duniani la Oktoberfest lilifungwa na polisi wa Munich ambao walikuwa wanashughulikia tishio la bomu na pia mlipuko unaoaminika kuhusishwa na mzozo wa kifamilia, ambapo mtuhumiwa alikutwa amekufa kwenye eneo la karibu.

Polisi wamesema mwanamume wa kijerumani mwenye umri wa miaka 57 aliyeichoma moto nyumba ya familia yake, alitoa tishio la bomu kulilenga tamasha la Oktoberfest alikufa baada kilipuzi alichokuwa amebeba kwenye mkoba wake kulipuka.

Kikosi cha kutegua mabomu kimeongeza kuwa mtu huyo alikufa kwa kujitoa mhanga kwenye shambulio, ambalo limesababisha mama yake mwenye umri wa miaka 81 na binti yake wa miaka 21 kujeruhiwa.

Taarifa kwenye tovuti ya jiji la Munich imesema uamuzi wa kuufunga uwanja kunakofanyika tamasha hilo ulichukuliwa kutokana na tishio la hilo la bomu lililoripotiwa huko kaskazini mwa Munich.

Ujerumani Munich 2025 | Tamasha la Oktoberfest
Tamasha maarufu la Oktoberfest huhudhuriwa na watu karibu milioni sita kila mwakaPicha: Felix Hörhager/dpa/picture alliance

“Kutokana na kilichotokea hapa Lerchenau, tunayachunguza maeneo mengine mjini Munich. Eneo la Theresienwiese pia limeathirika ambako tulipokea vitisho vya bomu na kwa sasa hatua za kuweka vizuizi zimechukuliwa. Wafanyikazi na wageni wote katika uwanja wa tamasha wameombwa kuondoka. Tamasha hilo litafunguliwa tena jioni hii, amesema msemaji wa Polisi wa Munich, Thomas Schelshorn.” 

Tamasha la Oktoberfest linalofanyika kila mwaka mjini Munich linatarajiwa kukamilika Oktoba 5, limekuwa likiendelea kuvutia umati wa kimataifa, na idadi kubwa ya wageni huwa wanatoka Marekani, Austria, Italia na Ufaransa.

Tamasha la Oktoberfest lilianza lini?

Lilianza mwaka wa 1810 kwa lengo la kuadhimisha harusi ya Mwanamfalme Ludwig wa Bavaria na Binti Mfalme Therese wa Saxony-Hildburghausen. Tamasha maarufu la Oktoberfest huhudhuriwa na watu karibu milioni sita kila mwaka.

Mnamo mwaka 1980 tamasha la Oktoberfest lilikabiliwa na shambulio baya la Wanazi mamboleo. Shambulio la bomu lililofanyika jioni ya Septemba 26, mwaka huo wa 1980, lilisababisha vifo vya watu 13, wakiwemo watoto watatu na mshambuliaji, mwanafunzi aliyeitwa Gundolf Koehler, aliyekuwa mfuasi wa kundi la mrengo wa mkali wa kulia lililopigwa marufuku. Zaidi ya watu 200 walijeruhiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *