Haki ya kura ya turufu ni mojawapo ya masuala yenye utata kuhusu mamlaka ya wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Haki ya kura ya turufu, inayohodhiwa na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (Marekani, Russia, China, Ufaransa na Uingereza), inampa kila mmoja wao mamlaka ya kuzuia azimio lolote au uamuzi wowote wa kiutendaji wa baraza hilo, bila kujali kiwango cha uungwaji mkono kutoka kwa nchi zingine.

Katika hali ambayo, watetezi wake wanaona kuwa ni chombo cha kudumisha amani na kuzuia migogoro kati ya mataifa makubwa, lakini kuna sababu nyingi za msingi za kuamini kwamba, kura ya veto si ya haki na ni kinyume kabisa na kanuni za msingi za usawa wa mataifa, uwajibikaji na utawala wa sheria. Jambo hili linaweza kutathminiwa katika mihimili kadhaa mikuu:

 Mosi: Ukiukaji wa kanuni ya haki sawa kwa mataifa yote.

Mkataba wa Umoja wa Mataifa umejikita juu ya msingi wa ” haki sawa wa wanachama wote.” Hata hivyo, haki ya kura ya turufu inakiuka kanuni hii ya kimsingi. Upendeleo huu unaugawa ulimwengu katika makundi mawili:

Kundi la kwanza ni la nchi tano za “daraja la kwanza” ambazo zina uwezo kamili wa kuzuia hatua na maamuzi ya kimataifa. Kundi la Pili ni la wanachama wengine 188 wa Umoja wa Mataifa ambao mamlaka yao hayajakamilika na yana mipaka ikilinganishwa na nguvu hizo tano.

Mfumo huu umeunda utawala wa utawala wa serikali ya wachache (oligarchy) katika kitovu cha taasisi muhimu zaidi ya usalama duniani, ambapo maslahi ya kitaifa ya nchi tano yanaweza kuchukua nafasi ya kwanza juu ya maslahi na matakwa ya wengi katika jamii ya kimataifa.

Pili: Kulemaza hatua muhimu za kimataifa wakati wa mgogoro.

Historia ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, mara nyingi nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama zimetumia kura yao ya turufu kulikwamisha baraza hilo kuchukua hatua zinazohitajika kuzuia majanga ya kibinadamu, kukomesha vita, au kuwafungulia mashtaka wahalifu. Mifano ya kihistoria inaonyesha ukosefu huu wa haki.

Miongoni mwa wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama, Marekani imetumia kura ya turufu zaidi kuliko wanachama wengine wanne wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kuanzia mwaka 1945 hadi Disemba 2023, Marekani imepiga kura ya turufu mara 89 kupinga maazimio ya Baraza la Usalama, huku mara 45 kati ya hizo yakihusiana na utawala wa Kizayuni wa Israel.

-Mgogoro wa Palestina: Marekani imekuwa ikitumia mara kwa mara kura ya turufu kumlinda na kumkingia kifua mshirika wake wa kimkakati, Israel, na imezuia azimio lolote la kulaani au takwa la kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na utawala vamizi wa Israel. Aidha katika kipindi cha miaka miwili ya vita vya Gaza, Washington mara kadhaa imetumia kura yake ya turufu kuzuia kulaaniwa utawala wa Kizayuni au kutoa wito wa kusitishwa vita hivyo.

Mgogoro wa Rwanda: Wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994, Marekani ilikataa kupitishwa maazimio ya kuimarisha ujumbe wa kulinda amani na kuzuia mauaji hayo, na kwa mukatadha huo kuzidisha maafa.

Mifano hii inaonyesha jinsi maslahi ya kijiografia ya nchi yanavyoweza kuzuia kuokoa maelfu ya roho au hata mamilioni ya uhai wa watu wasio na hatia.

Tatu: Kinga dhidi ya uwajibikaji na kudhoofisha utawala wa sheria.

Kivitendo haki ya veto inazipa kinga nguvu tano za nyuklia. Nchi hizi zinaweza kuendelea na vitendo vyao bila kuogopa hatua zozote rasmi za kimataifa kupitia Baraza la Usalama.

Moja ya vikao vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Kwa mfano, uvamizi wa Marekani nchini Iraq mwaka 2003. Licha ya kulaaniwa kimataifa, lakini Washington haikuwahi kukabiliwa na maazimio makali ya utekelezaji kutoka kwa Baraza la Usalama kutokana na uwezekano wa kutumia kura ya turufu. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, hii inadhoofisha kanuni ya utawala wa sheria, ambayo ni msingi wa utaratibu wa kimataifa, na kutuma ujumbe wazi kwamba, wenye nguvu wako juu ya sheria.

Nne: Kuakisiwa muundo wa nguvu ya ulimwengu ya mwaka1945, sio ulimwengu wa sasa.

Haki ya veto ni masalio ya muundo wa nguvu ya baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Ulimwengu wa sasa haufananishwi na ulimwengu wa 1945 wakati taasisi hiyo ilipoundwa. Kuibuka kwa nguvu mpya za kiuchumi na kisiasa kama vile India, Brazil, Ujerumani, Japan, Afrika Kusini na Nigeria, pamoja na kuongezeka kwa majukumu ya asasi kama vile Umoja wa Afrika, kumefanya haja ya marekebisho ya muundo wa Baraza la Usalama kuhitajika zaidi kuliko hapo awali.

Kuendelea ukiritimba wa mamlaka katika mikono ya nchi tano kunakanusha uwakilishi wa kweli wa jamii ya kimataifa na changamoto ya uhalali wa Baraza la Usalama na Umoja wa Mataifa.

Mintarafu hiyo, suala la kufanyika mabadiliko ya kimuundo katika Umoja wa Mataifa sambamba na matukio mapya ya kimataifa na kukomesha haki ya kura ya turufu ya madola matano ya kimataifa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linachukuliwa kuwa moja ya masuala mazito yanayotakiwa kuhusiana na haja ya kufanyika mageuzi katika chombo hicho kikubwa zaidi cha kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *