
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Jihadul Islami ya Palestina amekosoa vikali mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani wenye vipengele 20 wa eti kumaliza vita vya mauaji ya halaiki ya Israel dhidi ya Gaza, na kuutaja kama “mfumo wa kuendeleza uchokozi na uvamizi wa Israel dhidi ya taifa la Palestina.”
Ziyad al-Nakhalah amesisitiza kuwa, pendekezo hilo ambalo Trump aliliwasilisha katika Ikulu ya White House pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, linaakisi kikamilifu dira ya utawala unaokalia kwa mabavu wa Tel Aviv.
“Israel inalenga kutekeleza, kwa kuungwa mkono na Marekani, kile ambacho haikuweza kutimiza kupitia hatua za kijeshi. Kwa hiyo, tunaliona tamko la Marekani na Israel kama chachu ya kushadidish migogoro katika eneo hili,” Al-Nakhala ameeleza.
Afisa huyo mwandamizi wa Jihadul Islami amesema, “Makundi ya Muqawama katika eneo hili yanaliona pendekezo la Donald Trump kwa Gaza kuwa ni hatua ya hadaa ya kuuokoa utawala wa Kizayuni dhidi ya kushindwa katika vita vya Gaza.”
Wakati huo huo, Mohammed al-Farh, mwanachama mwandamizi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen, pia ameutaja mpango mpya wa Trump wa usitishaji vita huko Gaza kuwa usio wa haki na usiotekelezeka.
Amesisitiza kuwa, lengo la mpango huu ni kuwatenga Hamas na kupunguza hasira za umma duniani dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, na kwamba hauna utaratibu unaoweza kutekelezeka.
Kabla ya hapo, Mahmoud Mardawi, kiongozi wa Harakati ya Muqawama ya Hamas ya Palestina alisisitiza kwamba, mpango huo unaodaiwa ni wa eti kukomesha vita Gaza hauna maana yoyote wala mantiki.