Kipi kinafuata Iran baada ya kurejeshewa vikwazo?Kipi kinafuata Iran baada ya kurejeshewa vikwazo?

Kupitia kipengele cha kurejesha vikwazo ikiwa mchakato wa ukaguzi wa mpango wa nyuklia wa Iran utashindwa, maarufu kama “snapback” kwa lugha ya Kiingereza, vikwazo dhidi ya mauzo ya mafuta ya Iran, biashara ya silaha, na sekta ya benki vimerudishwa kikamilifu. Kipengele hicho ni sehemu ya makubaliano ya mwaka 2015 baina ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani, ambayo yaliparaganyika baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuiondoa nchi yake.

Hali hii imetokana na hatua ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuishutumu Tehran kwa kukiuka makubaliano hayo—ikiwemo kurutubisha kiasi kikubwa cha madini ya urani, kuwazuia wakaguzi wa kimataifa, na kukataa mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani.

Licha ya juhudi za China na Urusi kuchelewesha kurejeshwa kwa vikwazo hivyo, muda wa afuani wa siku 30 ulimalizika wiki hii. Sasa, Iran inakabiliwa na vikwazo ambavyo wataalamu wanaamini vitauathiri vibaya uchumi wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Kurejea kwa vikwazo vya ‘kausha damu’

Shahin Modarres ambaye ni mchambuzi wa masuala ya usalama, anasema hivi si vikwazo vya kawaida tu. anasema shughuli za kibenki zitatatizwa, mauzo ya mafuta yatabanwa, na hata biashara ya kawaida itazongwa na vizingiti. ”Kwa raia wa kawaida,” anasema mchambuzi huyo, ”hii inamaanisha mateso ya kila siku.”

Israel yaishambulia Iran na kulenga maeneo tofauti

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Thamani ya sarafu ya Iran inatarajiwa kuporomoka zaidi, na kufanya bidhaa za nje kuwa ghali mno. Ajira zitapotea, na mishahara itapungua thamani kutokana na mfumuko wa bei. Hali hii inasababisha kile ambacho wataalamu wa uchumi wamekipachika jina la ”faharasa ya machungu”, ambayo ni mseto wa ukosefu wa ajira na mfumko wa bei.

Je, diplomasia ya vikwazo yaweza kuleta suluhu?

Behrooz Bayat mwenye uraia pacha wa Ujerumani na Iran anaonya kuwa kurejeshwa kwa vikwazo kunaweza kuliuwa tabaka la kati ambalo ni mhimili wa demokrasia. Anasema ingawa hatimaye uongozi wa Iran unaweza kuanguka, hili litaigharimu nchi nzima, na hakutakuwa na faida yoyote kwa wananchi wa Iran.  

Wakati huo huo, njia za kidiplomasia zinaonekana kuwa finyu. Wanasiasa wa Magharibi wanasema wako tayari kwa mazungumzo, lakini Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Khamenei ameyatupilia mbali mazungumzo na Marekani akiyaita “njia isiyo na matumaini.”

Rais wa Marekani Donald Trump
Kuna hofu inayoongezeka nchini Iran kuwa yumkini Marekani ina azma ya kubadilisha uongozi mjini Tehran, Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Mchambuzi Shahin Modarres anasema utawala mjini Tehran unajua kuwa ukikubali kusitisha programu zake za nyuklia na makombora, utapoteza uungwaji mkono kutoka kwa kundi dogo lenye itikadi kali ambalo lina nguvu kubwa.

”Utawala huo uko tayari hata kupigana vita ili kudumisha mamlaka yake,” amesema Modarres.

Wasiwasi kuwa Marekani inataka kuipindua serikali ya Tehran

Kuna hofu inayoongezeka nchini Iran kuwa yumkini Marekani ina azma ya kubadilisha uongozi mjini Tehran, wakati jamhuri ya Kiiislamu ikiyumbishwa na vikwazo vilivyorejeshwa, na baada ya vita vya siku 12 na Israel. Hofu hiyo imechochewa na kauli ya balozi wa Marekani nchini Uturuki, Tom Barrack, ambaye wiki iliyopita alisema Iran na kundi la Hezbollah ni maadui wa Marekani, akizilinganisha na majoka ambayo lazima yakatwe vichwa.

Mtalaam wa masuala ya Iran Shahin Modarres haamini kuwa mtazamo huo wa Tom Barrack unatosha kufikiria kuwa Marekani imebadilisha sera yake juu ya Iran.

Kubadilisha utawala sio suala la porojo, anasema Modarres, na kuongeza kuwa ni hatua inayohitaji utashi wa kisiasa, na mpango mpana wa vita vitakavyoibuka, na kukubali kujitwisha athari zote zinazoweza kufuatia.

Wakati Iran ikijipata tena katika hali ya kutengwa, uongozi wake unaonekana kushikilia msimamo wake mkali.

Kwa kurejeshwa chini ya kipengele nambari saba cha mkataba wa Umoja wa Mataifa, taifa hilo la watu milioni 90 limevishwa tena nembo ya ”kitisho cha usalama na utengamano wa dunia.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *