
AGOA ulizinduliwa mwezi Mei mwaka 2000 kwa lengo la kusaidia nchi za Afrika kufikia soko la Marekani kupitia upendeleo wa kibiashara. Tangu wakati huo, mpango huo umesaidia sana mauzo ya bidhaa za kilimo, nguo na viwandani, na kuchochea ajira hususan kwa wanawake.
Mathalani nchini Lesotho, karibu theluthi moja ya mauzo ya nje yamekuwa yakitegemea AGOA, hasa katika sekta ya mavazi inayowaajiri kati ya wafanyakazi 30,000 hadi 40,000.
Kwa zaidi ya miaka 20 nchi zilizokuwa zikinufaika na AGOA ni pamoja na Kenya, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia Congo DRC, Afrika Kusini, Mauritius, Madagascar, Lesotho, Cape Verde, Guinea- Bissau, Comoros, Gambia pamoja na Sao Tome na Principe.
Mipango mipya ya Marekani kuhusu kodi
Tangu mwezi Aprili mwaka 2025, Marekani imeanza kutoza ushuru mpya wa bidhaa, hatua iliyopandisha viwango vya ushuru kutoka chini ya asilimia 0.5 hadi wastani wa asilimia 10 kwa nchi nyingi za AGOA. Bidhaa zilizoathirika zaidi ni pamoja na vyakula na mazao ya kilimo, vyuma, mashine, usafirishaji, pamoja na nguo na mavazi. Kwa baadhi ya sekta, ongezeko hilo limefikia viwango vya tarakimu mbili.
Kumalizika kwa AGOA mwezi Septemba 2025 kunamaanisha kuwa nchi 32 zilizokuwa zikifaidika na mpango huo sasa zitakabiliwa na ushuru maradufu, kwa kuwa badala ya upendeleo wa kibiashara, bidhaa zao zitalipishwa ushuru wa kawaida sambamba na ushuru maalumu kwa nchi au sekta husika.
Taarifa iliyochapishwa leo kwenye wavuti wa UNCTAD imeeleza kauwa “hali hii itakuwa pigo zaidi kwa nchi ambazo zimewekeza katika viwanda, hususan vya mavazi na bidhaa za chakula kilichosindikwa kama samaki na matunda yaliyokaushwa.”
Kwa upande mwingine, wauzaji wa mafuta na madini, kama vile nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo- DRC, Nigeria na Angola, hawataathirika sana kwa kuwa bidhaa zao tayari zinatozwa ushuru mdogo au hazihusishwi na ushuru mpya.
Shirika hilo la UN limebainisha kuwa nchi zenye uchumi ulio na mchanganyiko mkubwa, “mfano Afrika Kusini, zimepata athari za mapema mwaka huu kutokana na ushuru maalumu, japokuwa utegemezi wao kwa AGOA si mkubwa ikilinganishwa na majirani zao.”
Yote kwa yote, bila kuongezwa muda wa AGOA, juhudi za Afrika kuondokana na utegemezi wa kuuza malighafi pekee na badala yake kuwekeza kwenye bidhaa za kilimo na viwandani zitakumbwa na changamoto kubwa.
Je ungependa kujua kwa kina takwimu zinaeleza nini iwapo mpango wa AGOA utakufa kabisa? UNCTAD wamechapishwa maelezo ya kina ya kitaalamu ambayo unaweza kusoma kwa kubofya hapa