Kadiri jinai na mauaji ya kimbari ya Israel yanavyozidi kuongezeka huko Ghaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Lebanon ndivyo ususiaji wa kimataifa unavyozidi kushika kasi na sasa hivi mashirika ya silaha ya utawala wa Kizayuni yanakabiliwa na janga la kusambaratika kutokana na uvundo wake kuhinikiza kila sehemu duniani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, sekta ya silaha ya Israel imelemewa na janga la kuporomoka kwa mwezi wa ishini sasa kutokana na jinai zake huko Ghaza. Shirika hilo limenukuu tathmini ya mmoja wa wasimamizi wa sekta ya silaha ya Israel akiliambia gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth kuwa, iwapo hali ya hivi sasa na hasa sera za kuendeleza vita za baraza la mawaziri la Netanyahu zitaendelea, kuna uwezekano mkubwa sekta ya silaha ya Israel ikasambaratika mwaka 2026 na itapata na pigo kubwa na chungu mwaka 2027.

Jinai za utawala wa Kizayuni za mauaji ya umati Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Lebanon zimezifanya nchi nyingi duniani kuacha kununua silaha za Israel kutokana na kuhofia mashinikizo ya umma ndani ya nchi hizo na kuharibu sifa zao kimataifa.

Malalamiko ya kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni kutokana na jinai na mauaji yanayoendelea huko Ghaza, zimezifanya nchi nyingi duniani kutazama upya ushirikiano wao wa kiusalama wa kijeshi na Tel Aviv na kusimamisha au kufuta kabisa mikataba yao ya silaha na utawala huo ghasibu. Kwa mfano, hivi karibuni tu serikali ya Uhispania ilifuta mkataba wa silaha na kampuni ya kijeshi ya Israel ya Rafael wenye thamani ya zaidi ya dola milioni 218. Hatua hii ilichukuliwa kwa mujibu wa maamuzi ya Uhispania ya kusitisha kandarasi zenye thamani ya takriban dola milioni 654 na makampuni ya Israel katika miezi ya hivi karibuni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *