Kuna msemo wa Kiswahili usemao “Njaa mwanaharamu’ hii ikimaanisha kuwa ukiwa na jaa unaweza kufanya hata yale unayojua fika hayapaswi kufanywa lakini ufanyaje sasa na ndio una njaa?

Kauli hii inabeba uhalisia wa maisha ya wakazi wa Gaza katika eneo la Deir al-Balah.

Huyu ni Umm Mohammed Al-Masri, akiwa amezungukwa na watoto wake wadogo walishika plastiki nyepesi ili kumpa kuchochea moto wakati akipika chapati. Anazungumza akionesha Inhaler, kifaa cheye dawa ya kupuliza kwa ajili ya kusaidia kupumua kwa watu wenye magonjwa ya kupumua kama pumu.

“Kifaa hiki ndio pumzi yangu, nilikuwa nimebanwa na kupumua, watoto wangu wote walianza kupiga mayowe na kunikimbiza hospitali. Daktari alinipa kifaa hiki na alisema kitadumu kwa siku 15 lakini sasa ni siku ya tatu na ninahitaji kipya maana hiki nakitumia zaidi ya mara 15 kwasiku na hii ni sababu ya moshi kutoka katika jiko hili.”

Video ya Umoja wa Mataifa inamuonesha mama mwingine, Aisha Al-Ra’i mjamzito wa miezi nane akipika mkate katika jiko linalotumia taka za plastiki. Pembeni yake mtoto wake mdogo umri wake kama miaka mitatu hivi akimuangalia mama yake anayezungumza huku machozi yakimtoka.

“Unajua jinsi hali ya maisha ilivyo ngumu, na hatuna la kufanya. Nina mimba ya miezi minane, na ninakaa siku nzima mbele ya moto na moshi. Binti zangu huamka asubuhi na mapema ili kukusanya kuni na plastiki ili tupate chakula chetu cha kila siku na kuishi kama watu wengine. Tunamshukuru Mungu katika hali zote na tunamuomba ugumu huu uondolewe kwetu ili tuweze kurudi kwenye maisha yetu. Tunatumai hali ya maisha itaboresha.”

Hali ni hivyo hivyo kwa mama mwingine huyu aitwaye Umm Mohammed Abu Zuaiter, ambaye mbali ya kuwa mumewe ni mgonjwa kutokana na kutumia majiko haya yasiyo bora kwa afya zaidi ya miaka 10 sasa, naye pia anasumbuliwa na anasumbuliwa na shinikizo la damu na kisukari. Ramadhani iliyopita alipata ugonjwa wa kiharusi, na sasa Umm ni magonjwa ya mfumo wa kupumua.

Tuelekee hospital ya Al-adsa, Dkt Kjalil Al-Daqran ambaye ni msemaji wa Wizara ya afya ya Gaza anasema

“Wakati Israel ikiendelea kufunga vivuko na kuzuia kuingia kwa mafuta na gesi ya kupikia, wanawake katika Ukanda wa Gaza wameamua kutumia karatasi na taka za plastiki kupika chakula na kuoka mikate. Hii imesababisha utoaji wa moshi wenye sumu na kusababisha kuenea kwa magonjwa ya kupumua na kusababisha hatari kubwa ya afya ya umma katika Ukanda huu. Hospitali za Gaza haziwezi kutoa huduma za afya kwa wagonjwa hao kutokana na ukosefu wa dawa na vifaa muhimu vya matibabu. Hali hii inahitaji uingiliaji kati wa haraka kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na mashirika ya kimataifa kuishinikiza Israel kuruhusu kuingia kwa dawa muhimu, vifaa vya matibabu, mafuta na chakula ili kuokoa maisha ya watu katika Ukanda wa Gaza.”

Juhudi za kumaliza vita vinaendelea unaweza kutembelea wavuti wetu ambao ni news.un.org kusoma taarifa ya mpango mpya wa Marekani wa kumaliza vita Gaza wenye vipengele 20, mpango ambao Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anaupigia chepuo ukubaliwe na pande zote za kwenye mzozo.

Soma taarifa hiyo hapa

Topic: Afya

Tags: Gaza, Israel, wanawake katika mizozo, mazingira 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *