Makundi ya Muqawama katika eneo hili la Asia Magharibi yakiwemo ya Jihadul-Islami ya Palestina na Ansarullah ya Yemen yameuelezea mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani kwa ajili ya Ghaza kuwa ni jaribio la kutapatapa la kuuokoa utawala wa kizayuni wa Israel usishindwe katika vita vya mauaji ya kimbari ulivyoanzisha dhidi ya eneo hilo la Palestina uliloliwekea mzingiro.
Ziad al-Nakhala, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesema, taarifa aliyotoa Trump mbele ya wanahabari akiwa pamoja na Netanyahu ni mpango wa utawala wa Kizayuni na ni waraka wa agizo la kuendeleza uchokozi na uvamizi dhidi ya wananchi wa Palestina.
Al-Nakhalah amefafanua: “huu ni waraka wa agizo la kuendeleza uchokozi dhidi ya watu wa Palestina; na Israel inajaribu kupata kupitia Marekani kile ambacho haijaweza kukipata kupitia vita”.
Katibu Mkuu wa Jihadul-Islami ameongezea kwa kusema: “sisi tunauchukulia mpango huu wa Marekani na Israel kama hati za kuliingiza eneo kwenye hali ya mripuko”.
Mohammed al-Farah, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen yeye amesema, mpango wa Donald Trump kwa ajili ya Ghaza ni wa kiuonevu na hautekelezeki.
Al-Farah, amesisitiza kwamba: “mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani hautekelezeki na lengo lake ni kuitupa nje ya ulingo Hamas na kuifanya ionekane kuwa ndiyo inayobeba dhima ya vita”.
Afisa huyo wa Ansarullah ya Yemen ameongeza kuwa, mpango huo wa Trump unalenga kupunguza hasira za walimwengu dhidi ya Israel na kufuta mshikamano wa ulimwengu na Palestina.

Mpango wa Trump wa vipengele 21 kuhusu Ghaza unaonekana na wachambuzi wengi na makundi ya Muqawama wa Palestina kuwa ni jaribio la kuuokoa utawala wa kizayuni na kushindwa kijeshi na kisiasa katika vita vya Ghaza.
Utawala wa kizayuni umeshindwa kufikia malengo yake ya kijeshi katika vita vya Ghaza, ikiwemo kuiangamiza miundombinu ya Muqawama, kuwakomboa mateka wa kizayuni, au kurejesha usalama katika vitongoji haramu vya walowezi wa kizayuni karibu na Ghaza. Ukweli ni kwamba mpango wa Trump ambao umejikita katika kuipokonya silaha Hamas na kuikabidhi Ghaza kwa taasisi za kimataifa, ni jaribio la kuyafikia malengo hayo yote kwa njia za kisiasa.
Mpango huo unataka kupokonywa silaha kikamilifu makundi ya Muqawama wa Palestina na kutoshirikishwa kwenye uendeshaji wa Ghaza, ikiwa ni ithibati kwamba utawala wa kizayuni na Marekani zinataka kuwatokomeza wadau na wahusika wakuu wa mapambano ya ukombozi wa Palestina baada ya kushindwa kufanya hivyo katika medani ya vita.
Kwa mujibu wa mpango wa Trump, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair amepangwa kuwa liwali wa muda wa Ghaza na atasimamia taasisi itakayoitwa Mamlaka ya Kimataifa ya Mpito ya Ghaza, “Ghaza International Transitional Authority” au GITA. Pendekezo la kuanzishwa taasisi hiyo ya GITA ikiwa chini ya uongozi wa Blair, ambaye ana rekodi ya kuwa na uhusiano wa karibu na utawala wa kizayuni na Marekani, linadhihirisha njama inayojaribiwa kufanywa ya kuidhibiti Ghaza kupitia taasisi ya kimataifa yenye mfungamano na nchi za Magharibi. Hii ni hila ya kuyapiga chenga matakwa ya wananchi wa Palestina na Muqawama wao.
Pendekezo la kuwahamisha wakazi wa Ghaza na kuwapeleka nchi nyingine kama vile Jordan na Misri nalo pia limetafsiriwa na makundi ya Muqawama kama “maangamizi ya kizazi” na “kufukuzwa kwa mabavu”.
Mpango wa Trump hauna ratiba maalumu ya kuondoka jeshi la utawala wa kizayuni katika maeneo linayoyakalia kwa mabavu huko Ghaza. Jambo hili limeyafanya makundi ya Muqawama yaichukulie hatua hiyo kuwa ni hila tu ya kisiasa ya kupunguza mashinikizo ya kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Kwa mtazamo wa makundi ya Muqawama, mpango wa Trump sio tu hautatui mgogoro uliopo, lakini pia ni jaribio la kuuokoa utawala wa Kizayuni usishindwe katika vita vya Ghaza na kulazimisha matakwa ya Marekani na utawala wa Kizayuni kwa wananchi wa Palestina. Badala ya mpango huo kukomesha ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na utawala wa Kizayuni, utazidi kuendeleza tu mchakato huo.

Kwa mtazamo wa makundi ya Muqawama wa Palestina na wachambuzi wengi wa mambo, mpango wa Trump wa vipengele 21 kwa ajili ya Ghaza si hakikisho la kupatikana haki za kisheria za wananchi wa Palestina, kwa sababu muundo, maudhui na malengo yake yamepuuza matakwa ya kihistoria, ya kibinadamu na ya kisheria ya Wapalestina; na unachojali zaidi ni maslahi ya utawala wa kizayuni na Marekani.
Mpango huo wa Trump umeandaliwa bila kuwashirikisha kwa maana halisi Wapalestina na haujazingatia ndani yake kuweka utaratibu wowote wa kupata maoni ya watu wa Ghaza au Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Huu ni ukiukaji wa wazi wa kanuni ya msingi ya sheria za kimataifa, yaani, “haki ya mataifa kujiamulia mustakabali wao.” Mpango huo unataka makundi ya Muqawama yapokonywe silaha kikamilifu, lakini hautoi hakikisho lolote la kukomeshwa ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na utawala wa Kizayuni, kusimamishwa ujenzi haramu wa vitongoji, au kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika makazi yao ya asili. Mpango huo unaunyima Muqawama wa Palestina nyenzo za ulinzi bila ya kuwahakikishia Wapalestina usalama au mamlaka ya kujitawala.
Ndio kusema kuwa, mpango huo wa Trump umeandaliwa ili uwe zaidi ni wenzo wa kuuokoa utawala wa Kizayuni na kushindwa katika vita vya Ghaza na kutwisha nidhamu na utaratibu mpya unaozingatia maslahi ya Marekani na Wazayuni katika eneo, bila kutoa njia ya ufumbuzi ya haki na ya kiadilifu kwa mgogoro wa Palestina…/