
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian ameashiria azma na irada thabiti ya Jamhuri ya Kiislamu mkabala wa mashinikizo ya maajinabi na kutangaza kwamba, taifa hili kamwe halitakubali kuburuzwa na kushinikizwa.
Akizungumza jana Jumanne katika hafla ya kuienzi timu za taifa za mieleka mtindo wa freestyle na Greco-Roman kwa kutwaa ubingwa wa dunia nchini Croatia hivi karibuni, Pezeshkian amewapongeza wanamieleka hao kwa kuwa kiigizo chema kwa vijana wa nchi hii.
“Mnaweza kuwa mfano wa kuigwa na kizazi cha vijana kupitia mwenendo na tabia zenu,” amesema Dakta pezeshkian na kusisitiza kuwa Iran bado imesimama kidete licha ya changamoto zinazoongezeka kila uchao.
Raia wa Iran amebainisha kuwa, “Ulimwengu unatushinikiza kujisalimisha, lakini kujisalimisha sio dhati na asili yetu. Tutasimama kwa ajili ya Iran hadi pumzi ya mwisho na hatutainamisha vichwa vyetu.”
Rais amegusia vikwazo vya kiuchumi na vizuizi vilivyowekewa nchi hii, akisisitizia haja ya kutegemea uwezo wa ndani. “Tunapotumia uwezo wetu, hakika tutafikia malengo yetu,” ameongeza.
Katika matamshi kama hayo siku ya Jumatatu, Rais Pezeshkian alisema maadui wanatafuta kuiwekea vikwazo Iran kwa sababu nchi hii imekataa kudhalilishwa na kupigia maadui magoti.
“Wanataka kutulazimisha kujisalimisha kwa watu duni na waovu, lakini hata kufikiria hilo halina nafasi akilini mwangu,” Pezeshkian alisema na kusisitiza kuwa, kuipigisha magoti Iran na watu wake ni ndoto za alinacha.