
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wanachama wote wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla wajitokeze kwa wingi Oktoba 29 na kwenda kupiga kura, na wasikubali kushawishika kuvunja amani ya nchi.
Samia ameyasema hayo Oktoba 1, 2025, wakati wa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu, katika mji wa Bomang’ombe wilayani Hai Mkoa wa Kilimanjaro, akiwa njiani kuelekea Arusha.
Mgombea huyo, amewahimiza wana CCM na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuinyanyua CCM ili wanaoitazama Tanzania kwa jicho lingine ‘waweke heshima’.
“Tukipiga kura kwa wingi, tukiinyanyua CCM kwa wingi, wale wanaoitazama Tanzania kwa jicho lingine wataweka heshima sawasawa,” alisema Samia.
Ameongeza: “La pili ninalotaka kuwaambia ndugu zangu msikubali kushawishiwa, mkikubali kushawishiwa tutaharibu amani ya nchi yetu ya Tanzania. Msikubali hata kidogo”.