
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amezungumzia njama za maadui dhidi ya taifa la Iran na kusisitiza kwa kusema: “Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba tutatoa pigo zito zaidi, tata na kali mno dhidi ya adui kuliko huko nyuma, iwapo kutaanzishwa vita vipya dhidi yetu.”
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Brigedia Jenerali Ali Mohammad Naeini, amesema hayo usiku wa kuamkia leo Jumatano, Oktoba Mosi, 2025 kwenye kipindi cha televisheni cha “Majira ya Palestina,” akisisitizia umuhimu mkubwa sana wa kupata nusra ya Allah na mwongozo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kuleta mshikamano kwenye jamii ya Iran wakati wa vita vya siku 12 vya hivi karibuni. Amesema: Adui hakutoeheka tu na vita vya kijeshi, bali aliendesha pia vita vya welewa, kujitambua na vita vya kisaikolojia. Alishambulia pia uchumi, masuala ya kijamii na utulivu wa kisaikolojia wa jamii ya Iran, lakini ameshindwa.
Brigedia Jenerali Naeini ameongeza kwa kusema: “Adui anajaribu kuiweka Iran katika hali ya kutokuwa kwenye vita na kutokuwa kwenye amani ili kujaribu kuathiri utulivu wa kiuchumi na wa kisaikolojia wa wananchi wetu.”
Msemaji wa Jeshi la SEPAH pia emesema, “adui alianzisha vita akiwa na malengo ya juu kabisa na alijiandaa kikamilifu kwa nguvu zake zote lakini ameshindwa.
Amesema: “Utawala wa Kizayuni na wafuasi wake hawana uwezo wowote mwingine wa kuanzisha vita vipya. Wakati wa vita vya siku 12, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH lilitumia sehemu ndogo tu ya uwezo wake na kufelisha njama za adui.”
Amesema, kikosi chetu cha anga ndicho hasa kilichoingia vitani. Sehemu kubwa ya Jeshi la SEPAH na vikosi vingine vya ulinzi vya Iran havikuingia uwanjani kwa sababu hakukuwa na ulazima wa kufanya hivyo.”
Aidha amenukuu maneno ya shahidi Hajj Qassem Soleimani kwamba “migogoro na vita hutengeneza fursa,” na kusisitiza kuwa, “Adui kwa upumbavu na ujinga wake ametupa fursa ya kutambua na kurekebisha udhaifu na kuimarisha nguvu zetu. Tumeweza kujua zaidi udhaifu wa adui. Baada ya vita vya siku 12, makamanda wa SEPAH wanafanya kazi usiku na mchana kuboresha nguvu zetu za ulinzi, kupanga mipango ya ubunifu na kujiweka tayari kulilinda taifa.”