
Taarifa kutoka nchini Uingereza zimefichua kuwa, nchi hiyo ya kifalme ya Ulaya iliupa utawala wa Kizayuni risasi 110,000 ndani ya mwezi mmoja tu ili Israel iendelee kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
Channel 4 ya televisheni ya Shirika la Utangaza la Uingereza imeripoti kuwa, shehena hiyo ya silaha yenye thamani ya karibu dola 27,000 ilipewa Israel mwezi Agosti mwaka huu. Hiyo ni sehemu ya ongezeko kubwa la mauzo ya silaha za Uingereza kwa Israel.
Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema: “Uchambuzi wetu wa takwimu za Mamlaka ya Ushuru ya Israel unaonesha kuwa, silaha zenye thamani ya karibu £400,000 ziliwasili Israel kutoka Uingereza mwezi Juni 2025. Hicho ni kiasi cha juu zaidi cha silaha za Uingereza kupewa katika kipindi cha mwezi mmoja. Rekodi hiyo ilikuwa haijavunjwa kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita,” imesema taarifa ya shirika hilo la utangazaji la Uingereza.
Mwezi Septemba, serikali ya Uingereza ilisimamisha leseni 30 kati ya 350 za kuuza silaha nje ya nchi baada ya kubaini hatari ya wazi ya “ukiukaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu.”
Hata hivyo ripoti ya vuguvugu la vijana wa Palestina, Progressive International na Workers for a Free Palestine ilifichua mapema mwaka huu kwamba serikali ya Uingereza inaendelea kuusheheneza silaha utawala wa Kizayuni wa Israel licha ya kupigwa marufuku kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Uingereza imeipa Israel silaha 8,630 tofauti tangu baada ya kutolewa marufuku hiyo. Silaha hizo zimejumnuisha mabomu, maguruneti, makombora na zana nyingine mbalimbali za kijeshi.
Uingereza inalalamikiwa vikali kimataifa kwa kushiriki moja kwa moja kwenye jinai za Israel hata baada ya tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuthibitisha Septemba 16 mwaka huu kwamba utawala wa Kizayuni unatumia silaha hizo kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Ghaza.