
Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) alisema jana Jumanne kwamba, azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa mapigano mashariki mwa nchi hiyo lazima litekelezwe.
“Amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo bado ni jukumu letu kubwa. Kuna hitilafu kati ya maendeleo tunayoyaona kwenye karatasi na ukweli tunaouona ardhini. Ukweli tunaouona ardhini unaendelea kugubikwa na ghasia,” amesema Bintou Keita, mwakilishi maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Udhibiti wa Mambo nchini DRC (MONUSCO).
Azimio nambari 2773 la Baraza la Usalama lililopasishwa Februari 21, linasema kwamba kundi la Machi 23 (M23) linapaswa kusitisha vita mara moja, lijiondoe katika maeneo yote liliyoyateka na kubatilisha kikamilifu tawala zisizo halali zilizoanzishwa na waasi hao huko mashariki mwa DRC.
Bi Keita pia amesema: Licha ya kupita miezi kadhaa lakini bado vifungu muhimu vya Azimio 2773 havijatekelezwa. Bado Muungano wa Congo River Alliance (AFC)-M23 umeendelea kuteka na kujiimarisha kwenye maeneo mengi zaidi.
Aidha ameliambia Baraza la Usalama katika mkutano mfupi kwamba: “Tangu AFC-M23 ilipoiteka Goma, imebadilisha taasisi rasmi katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini na kuzifanya dhaifu. Zaidi ya wanajeshi wapya 7,000 wamepitia mafunzo ya kijeshi katika kipindi cha miezi saba iliyopita kwenye kambi za AFC-M23.”
Timu ya Umoja wa Mataifa huko DRC (MONUSCO) inajulikana hivyo kwa kifupi chake cha lugha ya Kifaransa. Bi Keita amesema: “MONUSCO inaendelea kujitolea kikamilifu kuunga mkono juhudi zinazoendelea za kurejesha amani na iko tayari kutekeleza jukumu lake katika kuunga mkono utekelezaji wa usitishaji vita wa kudumu, mradi tu itapata mamlaka ya wazi kutoka kwa Baraza la Usalama na rasilimali kuendana na matarajio.”