Serikali ya Venezuela imetangaza kuwa itaamilisha “Dikrii ya Dharura ya Kigeni” ikiwa Marekani itaanzisha mashambulizi yoyote ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo.

Amri hiyo itampa Rais Nicolás Maduro mamlaka maalum ya kulinda amani na usalama wa taifa. Chini ya dikrii hiyo, Rais Maduro ataruhusiwa kukusanya na kuviweka tarayi Vikosi vya Wanajeshi wa Kitaifa vya Bolivia kote nchini.

Katika mkutano na wanadiplomasia wa kigeni huko Caracas, Makamu wa Rais wa Venezuela, Delcy Rodríguez amesisitiza kwamba, amri hiyo ina msingi thabiti katika Katiba ya Venezuela na sheria za kimataifa, haswa Kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa, ambacho kinasisitizia haki ya mataifa ya kujilinda katika tukio la shambulio la silaha.

Rodríguez amewaambia mabalozi kuwa: “Ikiwa Marekani inataka pipa la mafuta au molekuli ya gesi, lazima ilipie. Rasilimali hizi ni matokeo ya jitihada za watu wa Venezuela kuelekea maendeleo ya taifa na zinakusudiwa kutumikia mataifa yenye uhitaji, si mamlaka ambazo zinafuata sera za kijeshi dhidi ya ubinadamu. Hilo halitafanyika.” Amesisitiza kuwa, “Venezuela iko tayari kujihami na kujilinda.”

Hivi karibuni pia, Waziri wa Ulinzi wa Venezuela, Vladimir Padrino López alilaani kitendo cha Marekani cha kupeleka vikosi vyake vya majini kwenye visiwa vya Caribbean kwa kisingizio kupambana na ulanguzi wa mihadarati, akisisitiza kuwa lengo halisi la Washington ni kuangusha serikali halali ya Rais Nicolas Maduro.

Kabla ya hapo pia, Rais Maduro alionya kuwa, nchi yake itagura kutoka kwenye ‘siasa na diplomasia’ na kuingia kwenye “mapambano ya kutumia silaha” iwapo Marekani itaanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya taifa hilo. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *