
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetangaza kuwa jumla ya wapiga kura 717,557 ndiyo waliodhinishwa kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa uhakika wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Kulingana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina, jumla ya wapiga kura 8,325 wameondolewa katika daftari hilo kutokana na kukosa sifa.
Kati ya wapigakura waliodhinishwa, wanawake ni 378,334, ambayo ni sawa na asilimia 53, huku wanaume wakiwa 339, 223, sawa na asilimia 47.
Kati ya idadi hiyo, vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 ni 326,304(asilimia 45), wenye umri wa miaka 36 hadi 59 ni 300,986(asilimia 42) na walio na umri wa miaka 59 na kuendelea ni 90,267 ambayo ni sawa na asilimia 13.