Jinai za Marekani wakati wa kuikalia kwa mabavu Iraq zilikuwa kubwa na mfano mchungu sana wa mauaji na uharibifu chini humo ambazo wavamizi wa Kimarekani walijaribu na hadi sasa wanaendelea kujaribu kuzihalalisha kwa majina tofauti ya udanganyifu.

Kukaliwa kwa mabavu Iraq na Marekani kulianza mwaka 2003 kwa lengo la eti kuharibu silaha za maangamizi ya umati na kupambana na ugaidi. Lakini, uvamizi huo wa kijeshi uligeuka haraka kuwa mgogoro wa kibinadamu, kisheria na kisiasa, ambao athari zake mbaya zinaendelea kuitesa Iraq hadi leo hii. Jinai na uhalifu mkubwa zaidi uliofanywa na Marekani wakati wa kuikalia kwa mabavu Iraq ni pamoja na:

1- Mauaji mengi ya raia

Mauaji ya umati ya raia nchini Iraq yaliyofanywa na majeshi ya Marekani yalikuwa ni moja ya jinai kubwa na chungu zaidi za wakati wa kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo mwaka 2003. Jinai hizo hazikuwa janga kwa upande wa kibinadamu tu, bali pia ulikuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimsingi za kimataifa. Kwa mujibu wa ripoti za kuaminika, katika miaka mitatu ya kwanza ya kukaliwa kwa Iraq yaani kuanzia 2003 hadi 2005, karibu watu 655,000 walipoteza maisha. Idadi hiyo inajumuisha wahanga wa mashambulizi ya anga, operesheni za ardhini, mashambulizi ya anga ya kiholela na mapigano ya mitaani. Wengi wa wahanga hao walikuwa raia wa kawaida ambao walilengwa katika maeneo ya uraiani walikokuwa wanaishi. Aidha kufikia mwaka 2007, idadi ya wahanga wa uvamizi wa Marekani nchini Iraq ilikuwa imefikia karibu watu milioni moja. Kwa mujibu wa ripoti ya mashirika huru kama vile “Iraq Body Count”, zaidi ya raia 200,000 walikuwa wamepoteza maisha nchini Iraq kufikia mwaka 2023 kutokana na uvamizi wa Marekani. Idadi hiyo inajumuisha wahanga wa mashambulizi ya anga, operesheni za ardhini, miripuko ya mabomu, mapigano ya mijini na vitendo vya kigaidi vya wanamgambo wanaoungwa mkono na Marekani. Duru nyingine kama vile “Lancet” zimefikia hata kukadiria idadi ya vifo kuwa ni zaidi ya watu 655,000 katika kipindi cha miaka mitatu ya kwanza ya uvamizi na kukaliwa kwa mabavu Iraq na madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani. Licha ya kutolewa ushahidi mwingi, lakini cha kusikitisha zaidi ni kwamba, wengi wa wahusika wa jinai na uhalifu huo hawajawahi kufikishwa mahakamani. Marekani mara nyingi inakwepa kuwawajibisha wanajeshi wake na kudai kuwa makosa yao hayakufanywa kwa makusudi na yalikuwa ni makosa ya uendeshaji. Jambo hilo limedhoofisha mno imani ya wananchi wa Iraq kwa taasisi za kimataifa na mashirika yanayodai kupigania haki za binadamu duniani.

Mifano ya jinai za Marekani nchini Iraq

Mauaji ya raia huko Fallujah mwaka 2004: Maelfu ya raia wa Iraq waliuawa katika operesheni mbili kubwa za kijeshi. Wakati huo kulitolewa ripoti za matumizi ya fosforasi nyeupe na mabomu ya nyuklia iliyokhafifishwa katika maeneo ya makazi ya raia. Huo ulikuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za vita.

Mashambulizi ya anga ya kiholela: Katika nyakati nyingi tofauti, Wamarekani walifanya mauaji ya raia kwenye harusi, mazishi au mikusanyiko ya watu bila ya kujali kwamba ilikuwa ni mikusanyiko ya kiraia. Moja ya jinai hizo ni lile shambulio lililofanywa na Wamarekani kwenye harusi ya wananchi wa Iraq katika jimbo la Anbar. Jinai hiyo iliua zaidi ya watu 40 kwa mkupuo mmoja.

Mateso na jinai za kinyama zilitendwa na Wamarekani wakati walipoivamia Iraq

2-  Uharibifu wa miundombinu na huduma za jamii

Wanajeshi wa Marekani waliharibu vibaya miundombinu ya Iraq kwa kushambulia vituo muhimu kama vile mitambo ya kuzalisha umeme, viwanda vya kusafisha mafuta, hospitali na skuli. Jinai hizo si tu zilivuruga maisha ya kila siku ya watu, lakini pia zilileta mgogoro mkubwa katika ujenzi wa nchi. Ripoti zinasema kuwa, Iraq imeshatumia karibu dola bilioni 40 kufufua sekta ya nishati, lakini kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa na Marekani, hali ya sekta hiyo bado ni mbaya.

3- Mateso na vitendo vya kinyama kwa wafungwa

Kuenea picha za mateso ya wafungwa katika jela ya Abu Ghraib ilikuwa ni moja ya kashfa kubwa za uvamizi wa Marekani nchini Iraq. Wafungwa wa Iraq waliteswa kimwili na kisaikolojia, ikiwa ni pamoja na matumizi ya shoti za umeme, unyanyasaji wa kijinsia, udhalilishaji na kukoseshwa usingizi. Jinai hizo ni ukiukaji wa wazi wa Mikataba ya Geneva na sheria za kimataifa za haki za binadamu. Mbali na mateso ya kila upande, wafungwa wengine walikufa kwa kupigwa au kunyimwa huduma za matibabu. Picha zilizotolewa kutoka kwenye gereza hilo zilizua wimbi la ghadhabu ulimwenguni dhidi ya uvamizi wa Marekani huko Iraq.

4- Mgogoro wa wakimbizi

Uvamizi wa Iraq, mauaji na ghasia zilizofuatia uvamizi huo zilisababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, kufikia mwaka 2007, takriban watu milioni mbili walikuwa wamekimbilia nchi jirani kama vile Syria na Jordan, na zaidi ya watu milioni saba walilazimika kukimbia makazi yao ndani ya Iraq. Familia zilisambaratika, watoto walikuwa mayatima na vizazi vinatatizika na athari za kisaikolojia na kijamii za jinai hizo hadi leo hii. Mgogoro huu wa kibinadamu ni matokeo ya moja kwa moja ya uvamizi wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq.

5- Kuundwa na kuimarishwa magenge ya kigaidi

Wachambuzi wengi wa mambo wanaamini kuwa, siasa za Marekani nchini Iraq zilifungua njia ya kuundwa na kuimarishwa magenge ya kigaidi. Ombwe la usalama, ukosefu wa uthabiti wa kisiasa na ukandamizaji wa kikabila na kidini uliandaa mazingira ya kukua na kupata nguvu magenge ya kigaidi na ya misimamo mikali. Mfano wa wazi kabisa ni kupata nguvu genge la kigaidi la Daesh yaani ISIS ambalo kwa kukiri viongozi wenyewe wa Marekani, liliundwa na Wamarekani wakati wa utawala wa Barack Obama.

Hitimisho

Kiujumla ni kwamba jinai za Marekani nchini Iraq wakati wa kuikalia kwa mabavu nchi hiyo ya Kiarabu si tu ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, bali pia ulikuwa na madhara makubwa ya kibinadamu na kisiasa kwa watu wa Iraq na eneo hili zima. Kuanzia mauaji ya raia hadi uharibifu wa miundombinu, mateso kwa wafungwa na kuzushwa migogoro ya kibinadamu. Jinai hizo zitaendelea muda wote kubakia katika kumbukumbu ya kihistoria ya taifa la Iraq na kwamba mahakama za kimataifa zina wajibu wa kuchukua hatua dhidi ya jinai hizo. Uvamizi wa Marekani na kuikalia kwa mabavu Iraq ni moja ya sura za giza katika historia ya zama hizi ya Asia Magharibi. Jinai na uhalifu huu haukupoteza tu maisha ya mamia ya maelfu ya watu, lakini pia athari zake mbaya bado zipo katika jamii ya Iraq hadi leo hii.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *