Haya ndio unayopaswa kujua kuhusu Kikosi Kipya cha Kukabiliana na Magenge nchini Haiti au Gang Suppression Force – GSF.
GSF ni nini?
Kikosi cha Kukabiliana na Magenge GSF, nchini Haiti ni ujumbe mpya wa kimataifa ulioidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kwa kipindi cha mwaka mmoja, kikosi hicho chenye wanajeshi 5,550 kitafanya kazi sambamba na mamlaka za Haiti kudhibiti magenge, kulinda miundombinu, na kuwezesha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.
Lengo kuu ni kuwalinda watu walio hatarini dhidi ya ukatili unaoongezeka na kuzuia hali ya kulazimika kuyahama makazi yao isiyoepukika.

Polisi wa Haiti wakiangalia karatasi za dereva kwenye kituo cha ukaguzi.
Azimio la Baraza la Usalama limewasilishwa kwa pamoja na Panama na Marekani, likionesha msaada wa haraka wa kimataifa kwa mzozo wa pande nyingi unaoendelea nchini Haiti kwa miaka kadhaa sasa.
Malengo ya kikosi kipya ni yapi?
Malengo makuu ya kikosi hicho ni pamoja na kufanya operesheni za kijasusi au kiintelijensia kuvunja magenge yenye silaha, kulinda miundombinu muhimu, na kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu huku kikilinda raia.
GSF itashirikiana kwa karibu na mamlaka za Haiti, hasa polisi wa taifa, kwa nia ya kuweka mazingira ambapo Haiti itoweza kuchukua jukumu la usalama wake.
Pia, ujumbe huu unalenga kuimarisha taasisi za kitaifa na kuwezesha mazingira ya amani ya kudumu na maendeleo. Ofisi ya Usaidizi ya Umoja wa Mataifa itaanzishwa kutoa msaada wa kiufundi na kiutendaji.
GSF inachukua nafasi ya nani?
GSF inachukua nafasi ya Ujumbe wa Usaidizi wa Usalama wa Kimataifa MSS, nchini Haiti, hatua inayowakilisha mabadiliko ya kimkakati.
Ujumbe wa MSS, ukiongozwa na Kenya, ulilenga kusaidia polisi wa taifa wa Haiti lakini ulikuwa na wafanyakazi wachache na rasilimali finyu. Ulizinduliwa Oktoba 2023 huku kikosi cha kwanza kikianza kufika Juni mwaka uliofuata. Ujumbe huo ulisalia bila fedha za kutosha na haukuweza kupeleka kikosi cha watu 2,500 kilichoidhinishwa.
GSF itakuwa kikosi kikubwa zaidi, chenye nguvu na wigo mpana wa majukumu.
Kwa nini kinahitajiwa?
Kikosi kinahitajika haraka kudhibiti magenge kutokana na hali ya usalama isiyokuwa na mfano.
Vikundi vyenye silaha vinakadiriwa kudhibiti hadi asilimia 90 ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, vikifunga barabara, kushambulia miundombinu, na kuwatisha raia kupitia utekaji nyara kwa fidia, ubakaji na mauaji.

Kundi la genge hutembea katika kitongoji cha Port-au-Prince.
Zaidi ya watu 5,600 waliuawa mwaka 2024 pekee.
Tangu Machi 2025, ukatili umeenea hadi maeneo ambayo awali hayakuguswa nje ya mji mkuu, hususan maeneo ya Artibonite ambako watu 92,000 wamepoteza makazi na Centre ambapo watu 147,000 wamepoteza makazi.
Kwa jumla, zaidi ya watu milioni 1.3 wamelazimika kuhama, huku huduma muhimu kama afya na usambazaji chakula zikisambaratika.
Polisi wa taifa wa Haiti hawana uwezo wa kukabiliana na hali hiyo ipasavyo.
Kwa nini Haiti haiwezi kushughulikia tatizo hili peke yake?
Haiti haiwezi kushughulikia janga la magenge peke yake kwa sababu taasisi za serikali zimeporomoka, polisi hawana rasilimali, na ukatili ni mkubwa mno.
Magenge yameanzisha utawala wa kihalifu, yanatumia watoto, na kufanya biashara ya silaha pamoja na dawa za kulevya.
Umoja wa Mataifa umesisitiza mara nyingi kwamba kutokuwapo kwa adhabu,ukwepaji wa sheria, ufisadi, na kuanguka kwa taasisi ndizo sababu zinazochochea hali ya kutoaminika nchini Haiti.
Je, GSF itatatua matatizo ya Haiti?
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza kwamba usalama pekee hauwezi kutatua changamoto za Haiti.
Nchi inakabiliwa na migogoro mingi, mahitaji ya kibinadamu yanayochochewa na ukosefu wa usalama na majanga ya asili kama tetemeko la ardhi yanaongezeka, uchumi umeyumba, umasikini na kudorora kimaendeleo kumeenea, na hakuna serikali iliyochaguliwa tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moïse mwaka 2021.
Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wameeleza kuwa GSF lazima iwe sehemu ya mkakati mpana zaidi unaojumuisha mageuzi ya utawala, msaada wa kibinadamu, na maendeleo ya muda mrefu.
Kwa ufupi, GSF ni hatua muhimu lakini haitoshi, msaada wa kimataifa lazima uzidi usalama pekee ili kusaidia Haiti kurejea katika hali ya kawaida.
GSF itaanza lini kufanya kazi nchini Haiti?
GSF inatarajiwa kuanza kazi baada ya kumalizika kwa muda wa MSS kesho tarehe 2 Oktoba 2025, ingawa itachukua muda kujenga kikosi kipya kufikia idadi ya walinzi 5,500 pamoja na wafanyakazi wa kiraia 50 na kuanzisha ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukisaidia.
Haijabainika bado ni nchi zipi zitatoa wanajeshi. Azimio la Baraza la Usalama linaeleza kwamba kikosi kitafadhiliwa hasa kupitia michango ya hiari kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.