Russia imetangaza kuwa madai ya kurejesha vikwazo dhidi ya Iran hayana msingi wowote na hatua iliyochukuliwa na Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hilo inapingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Katika barua ndefu ambayo Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amemwandikia Katibu Mkuu wa umoja huo, Vasily Nebenzia amekosoa vikali hatua za hivi karibuni zilizochukuliwa na baadhi ya nchi za Magharibi na Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na “urejeshaji” vikwazo vya huko nyuma vya Baraza la Usalama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na akasisitiza kuwa hatua hizo hazina uhalali wowote wa kisheria na zinakwenda kinyume na Mkataba wa Umoja wa Mataifa na maamuzi ya Baraza la Usalama yenye ulazima wa utekelezaji.
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika UN ameeleza katika barua hiyo kwamba tangazo la Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa linalodai “kutekelezwa tena” maazimio 1696, 1737, 1747, 1803, 1835, na 1929 sio tu halina mashiko, lakini pia ni upotoshaji wa dhahiri shahiri wa maamuzi ya Baraza la Usalama na ukiukaji wa wazi wa Azimio 2231. Nebenzia ameongeza kuwa nchi tatu za Magharibi pamoja na baadhi ya nchi wajumbe wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama, zimesimama dhidi ya juhudi zilizolenga kutoa fursa zaidi ya mazungumzo kuhusiana na kadhia ya nyuklia la Iran na zimefadhilisha kutumia njia ya makabiliano na kushadidisha mivutano.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa ameashiria madai ya nchi tatu za Ulaya kwamba zilianza kutekeleza utaratibu wa “snapback” mnamo Agosti 28, na akasisitiza kuwa hatua hiyo haikuwa na itibari hata chembe. Amesema, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani sio tu hazikuzingatia masharti ya mchakato wa utatuzi wa mizozo yaliyoainishwa ndani ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, ambayo ni sehemu isiyotenganika na Azimio 2231, lakini kimsingi zimepoteza pia ustahiki wa kutekeleza utaratibu huo kutokana na ukiukaji wao wa mara kwa mara. Kwa maana hiyo, taarifa ya kuanza kwa mchakato huo wa “snapback” haina itibari yoyote ya kisheria na haiwezi kuchukuliwa kuwa ni taarifa halali kulingana na kifungu cha 11 cha Azimio 2231. Nebenzia amekumbusha kuwa, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Russia, China na Iran nao pia wametangaza rasmi msimamo huo katika barua yao ya pamoja ya Agosti 28 kwa Katibu Mkuu wa UN na Baraza la Usalama
Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika UN ameeleza pia alivyosikitishwa sana na hatua za Sekretarieti ya umoja huo, akisema zimechukuliwa kinyume na Kifungu cha 100 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa na msingi wa kutopendelea upande wowote unaopaswa kuheshimiwa na taasisi hiyo, na akaonya kwamba kuendelea kwa mwenendo huo kunaweza kudhoofisha mamlaka ya Baraza la Usalama. Amesisitiza kuwa hakuna msingi wa kisheria wa kuundwa upya Kamati nambari 1737 na kutekelezwa shughuli zinazohusika na kamati hiyo.
Balozi wa Russia ameitaka Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa ifute mara moja barua yake ya hivi karibuni, ibatilishe urejeshwaji wa orodha ya vikwazo, ifunge tovuti ya Kamati nambari 1737, na kujiepusha na hatua nyingine yoyote kwa ajili ya kukidhi maslahi ya madola machache ya Magharibi.

Russia inazichukulia kwa uzito mkubwa hatua za Troika ya Ulaya (Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani) ya kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran kuwa ni kitendo cha ukiukaji sheria kwa mtazamo wa sheria za kimataifa. Sababu kuu za msimamo huo uliochukuliwa na Moscow zinaweza kufupishwa katika nukta nne kuu:
1. Ukiukaji wa majukumu ya JCPOA na Azimio 2231
Russia inaamini kuwa, nchi za Ulaya na Marekani zenyewe zimekiuka wajibu na majukumu yao kulingana na makubaliano ya JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na hivyo kwa mujibu wa sheria za kimataifa, haziwezi kutumia nyenzo kama vile urejeshaji vikwazo dhidi ya Iran. Nchi hizo zinapaswa zichukue hatua ndani ya mpaka wa maazimio ya kimataifa au kulingana na makubaliano ya kimataifa yaliyofikiwa na pande kadhaa.
2. Utekelezaji haramu na wa kinyume cha sheria wa snapback
Russia imesisitiza kuwa, ‘snapback’ inaweza kuamilishwa na kutekelezwa katika hali iliyoainishwa tu, hasa kama Iran yenyewe itakuwa ndio upande wa kwanza kukiuka makubaliano ya JCPOA. Lakini Russia inaitakidi kuwa Iran haijakiuka majukumu yake katika nukta hizo, na kwa sababu hiyo, Ulaya haina haki ya kutekeleza ‘snapback’ kwa ajili ya kurejesha vikwazo.
3. Upinzani dhidi ya uwekaji vikwazo vya upande mmoja
Russia imeibua pia hoja ya kwamba vikwazo vya upande mmoja vilivyowekwa na baadhi ya nchi (hususan nje ya taratibu za kimataifa au Baraza la Usalama) ni kinyume cha sheria. Nchi hizo zinapaswa kuchukua hatua kulingana na maazimio ya kimataifa au makubaliano ya kimataifa ya pande kadhaa.
4. Ukiukaji wa misingi ya sheria za kimataifa
Kwa mtazamo wa Russia, nchi ambayo yenyewe haijatimiza ahadi ilizojikubalisha au imezipuuza haiwezi kutumia kisheria nyenzo kama vile vikwazo au kutekeleza utaratibu wa kisheria za kimataifa. Huo ni msingi unaotambulika katika sheria za kimataifa.
Na hitimisho la yote haya ni kwamba, kwa kutumia hoja hizo Russia inaitakidi kuwa, hatua za Troika ya Ulaya za kuamilisha na kutekeleza ‘snapback’ sio tu ni kinyume cha sheria lakini pia ni tishio kwa utulivu wa kikanda na kimataifa.
Lakini mkabala na msimamo huo, nchi za Ulaya na Marekani zinadai kuwa Iran haijatekeleza ahadi zake za nyuklia na kwamba urejeshaji wa vikwazo hivyo umefanywa kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama. Mgongano huo wa mitazamo umeibua changamoto kubwa za kisheria na kidiplomasia katika uga wa kimataifa. Kusema kweli, hivi sasa ndani ya Baraza la Usalama, kuna mgawanyiko na mpasuko wa wazi kabisa kati ya wanachama wa kudumu wa bara hilo. Russia na China, ambazo ni wapinzani wa ‘snapback’, zimesimama kukabiliana na watetezi wa Magharbi wa mpango huo, yaani Marekani, Ufaransa na Uingereza…/