Türk amesema kiwango cha ukatili na ukiukwaji wa haki kimefurutu ada, na kinahitaji msaada thabiti zaidi wa kimataifa kukidhibiti.

Amesisitiza kuwa “Tunaweza na lazima kubadili hali hii kwa ajili ya watu wa Haiti,” akiongeza kuwa  “bila hatua za haraka hali mbaya zaidi huenda ikaja kwa Haiti na eneo zima.”

Haiti yazongwa na ukatili wa magenge maelfu wameuawa

Tangu Januari 2022, zaidi ya watu 16,000 wameuawa na takriban 7,000 kujeruhiwa kutokana na ghasia za silaha na uhalifu wa magenge, kwa mujibu wa ufuatiliaji wa Umoja wa Mataifa.

Türk ameeleza jinsi magenge ya uhalifu yanavyosambaza hofu zaidi ya mji mkuu, Port-au-Prince, na kuingia vijijini huku yakitikisa jamii kupitia usafirishaji haramu wa silaha, unyang’anyi, utekaji nyara na ukatili wa kingono.

“Magenge yanatekeleza ukatili wa kingono kwa kiwango kikubwa ili kuonesha ubabe na ushawishi wa maeneo,” amesema Türk, akiongeza kuwa watoto wako katika hatari ya kutekwa, kulazimishwa kujiunga na magenge ya uhalifu na kunyanyaswa.

“Tunaweza kufikiria madhara ya muda mrefu, kwa watoto wa Haiti, na kwa jamii kwa ujumla.”

Athari zakibinadamu zinatia hofu, nusu ya wananchi wanahitaji msaada

Nusu ya watu wa Haiti ambao ni takribani watu milioni 6, wakiwemo watoto milioni 3.3 wanahitaji msaada wa kibinadamu, huku watu milioni 1.3 wakilazimika kuyahama makazi yao.

Nchi hiyo sasa ni miongoni mwa maeneo matano duniani yenye hali mbaya zaidi ya uhaba wa chakula. elimu pia imeporomoka, limeonya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF likiongeza kuwa mtoto mmoja kati ya saba yuko nje ya shule na karibu watoto milioni moja wako hatarini kuacha shule.

Hatua za serikali zazua wasiwasi

Türk pia amelaani matumizi makubwa ya nguvu na visivyo halali ya vikosi vya usalama vya serikali, akibainisha kuwa operesheni za polisi zinahusiana na zaidi ya nusu ya vifo na majeruhi mwaka huu.

Ameripoti kuwa vitengo maalum vya polisi vilitekeleza mauaji ya watu 174 mwaka huu, huku mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yakiua zaidi ya watu 550, wakiwemo watoto 11.

“Mashambulizi mengi ya ndege zisizo na rubani huenda si halali kisheria chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu,” amesema Türk, akionya kuwa mbinu hizo kali zinaweza kuchochea mzunguko wa ghasia.

Wito wa Msaada wa Kimataifa

Türk amekaribisha uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa Septemba 30 wa kuanzisha Kikosi cha Kukabiliana na Magenge nchini Haiti, akisema ni “ishara thabiti ya msaada wa kimataifa.”

Hata hivyo, amehimiza nchi wanachama kukisaidia kikosi hicho kwa rasilimali za kutosha, wafanyakazi, na kuhakikisha kinazingatia viwango vya haki za binadamu.

Ameongeza kuwa “Nchi zote zinapaswa kutekeleza vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya silaha kwa ukamilifu. Utekelezaji mipakani ni muhimu sana.”

Tunaweza na lazima kubadili hali hii’

Kamishna Mkuu amesisitiza kuwa juhudi za kurejesha usalama lazima ziende sambamba na kujenga upya mfumo wa sheria na haki nchini Haiti, kupambana na ukwepaji wa sheria na ukosefu wa usawa.

“Mamlaka, kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa, inahitaji kwa dharura kung’oa mizizi ya ufisadi na ukwepaji wa sheria, ikiwemo ndani ya taasisi za serikali,” amesema.

Amehitimisha kuwa “Watu wa Haiti wanahitaji umakini na msaada thabiti wa jumuiya ya kimataifa. Huu ndio wakati wa kuchukua hatua.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *