Leo ni Alkhamisi tarehe 9 Mfunguo Saba Rabiul-Thani 1447 Hijria Qamaria, sawa na tarehe 10 Mehr mwaka 1404 Hijria Shamsia, inayosadifiana na tarehe Pili Oktoba 2025 Miladia.

Siku kama ya leo, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya kihistoria, miaka 838 iliyopita, yaani Oktoba Pili, 1187, mji wa Baitul-Muqaddas ulikombolewa na Salahuddin Ayyubi kamanda wa wanamapambano wa Kiislamu. Awamu ya kwanza ya vita vya Msalaba baina ya Wakristo na Waislamu ilianza 1096 ambapo miaka minne baadaye majeshi ya Msalaba yaliushambulia mji wa Baitul-Muqaddas na kuukalia kwa mabavu. Wanajeshi wao wa Msalaba walifanya uporaji na kuwaua kikatili maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wasio na hatia wa ardhi hiyo. Hata hivyo mnamo mwaka 1187, baada ya Salahuddin Ayyubi kuidhibiti Syria, Lebanon na Misri, aliuzingira mji wa Baitul-Muqaddas. Awali aliwatumia ujumbe wavamizi akiwaeleza heshima maalumu anayoupa mji huo na kutotaka kufanya umwagaji damu katika eneo hilo na hivyo akawataka wavamizi hao waondoke katika mji huo na hata akawadhaminia usalama wa mali zao. Hata hivyo watu wa Msalaba walikataa na kupelekea kuibuka vita na mji huo kukombolewwa na Waislamu katika siku kama ya leo wakiongozwa na jemadari Salahuddin Ayyubi.

Baitul Muqaddas ulipo Msikiti mtukufu wa Al Aqsa

Miaka 156 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Mahatma Gandhi, kiongozi wa harakati ya kupigania uhuru nchini India katika moja ya vijiji vya jimbo la Gujarat. Mwaka 1891 Gandhi alirejea kutoka nchini Uingereza na kuishi mjini Mumbai. 1893 alisafiri kuelekea mjini KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini. Akiwa nchini humo Mahatma Gandhi alishuhudia ubaguzi wa rangi wa jamii ya wachache ndani ya taifa hilo. Mwaka 1917 na baada ya kurejea nchini kwake alipata umashuhuri mkubwa. Na miaka michache baada ya Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia yaani akiwa na umri wa miaka 33 Gandhi aliongoza mapambano kwa ajili ya kuwaokoa watu wake sanjari na kupigania uhuru wa India kutoka mikononi mwa Waingereza ambapo hatimaye na baada ya kuvumilia matatizo mengi akiwa pamoja na shakhsia tofauti kama vile Jawaharlal Nehru akafanikiwa kulipatia uhuru taifa hilo mnamo mwaka 1947 Miladia.

Mahatma Gandhi

Miaka 143 iliyopita katika siku hii, yaani tarehe 9 Rabi’ al-Thani, 1304 Hijiria, Ayatullah Hajj Mirza Abdul Rahim Nahavandi, mwanachuoni na faqihi mkubwa, alifariki dunia. Alikuwa na elimu na ujuzi mkubwa katika fiqhi na kanuni za fiqhi, na wanazuoni wengi na watu wenye hekima katika zama zake wa Iraq na Iran walinufaika na elimu yake. Inafaa kuashiria kwamba Ayatullah Nahavandi aliondoka katika mji wake wa Nahavand, magharibi mwa Iran, kuelekea mji wa Najaf huko Iraqi akiwa katika rika la ujana, na katika mji huu alinufaika kwa kuchota elimu kwa miaka mingi kwa maulamaa mashuhuri, hususan Sheikh Morteza Ansari, na katika muda wa miaka thelathini ya uhakiki na usomaji wa fiqhi na misingi yake, alifunza wanafunzi wengi sana ambao kila mmoja alifikia daraja za juu za elimu.

Miaka 143 iliyopita katika siku kama ya leo, tarehe 9 Rabi’ al-Thani 1304 Hijiria Qamaria aliaga dunia Ayatullah Sayyid Haidar Hilli akiwa na umri wa miaka 58. Abu al-Hasan Sayyid Haidar bin Sulayman bin Dawood Hilli Hussaini alikuwa akijulikana kuwa ni mmoja wa malenga na washairi watajika wa zama zake na akatambulika kama Imamu wa washairi wa Iraq. Alikuwa na fasaha ya uzungumzaji na uimara wa imani, na kutokana na kusanifu idadi kubwa ya mashairi ya kubainisha sifa na utukufu wa Ahlul-Bayt (a.s.), alikuwa maarufu kwa lakabu ya mshairi wa Ahlul-Bayt (a.s.). Miongoni mwa athari alizoacha malenga huyo ni Ad-Durr al-Yatim na Al-Aqdul-Mufassal. 

Tarehe Pili Oktoba miaka 121 iliyopita alizaliwa Graham Greene mwandishi wa Uingereza. Mwandishi huyo aliakisi matendo mema na mabaya katika athari zake na aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa ‘Nguvu na Utukufu’ kwamba subira, uvumilivu na mateso ni njia ya wokovu. Graham Greene amealifu vitabu vingi na baadhi yao ni ‘Mtu wa Tatu’, ‘Utawala Unaotisha’ na Muuaji wa Kukodishwa’. Mwandishi huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1991.

Na miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe Pili Oktoba 1958, nchi ya Guinea Conakry ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno walianza kumiminika nchini Guinea mwishoni mwa karne ya 15, na mwanzoni mwa karne ya 19, Wafaransa walipata satua zaidi nchini humo. Mwaka 1849 nchi hiyo ilikoloniwa rasmi na Ufaransa. Guinea Conakry inapakana na nchi za Senegal, Mali, Ivory Coast, Liberia, Sierra Leone na Guinea Bissau.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *