Mpira mpya unaotumika kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, umezua gumzo baada ya wachezaji na baadhi ya makocha kusema una kasoro.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi la Ligi (TPLB) hivi karibuni walitangaza kuwa sasa kuna mpira mpya ambao utakuwa unatumika na timu zote za Ligi Kuu Bara, mazoezini na kwenye mechi ikiwa ni mara ya kwanza kwenye ligi hiyo inayoshika nafasi ya nne kwa ubora Afrika.
Kabla ya hapo Ligi Kuu haikuwahi kuwa na mpira rasmi kama ilivyofanyika sasa, ambapo licha ya kwamba uzinduzi na utambulisho wa mpira huo ulifanyika wiki moja tangu kuanza kwa Ligi Kuu na hivyo kufanya baadhi ya timu kutowahi hata kuufanyia mazoezi, ila ndio unaendelea kutumika.
Hata hivyo, wakati ukiendelea kutumika, mpira huo umegeuka gumzo baada ya baadhi ya wachezaji na makocha kuulalamikia kwa madai kuwa una ubora tofauti na mipira waliyoizoea, huku washambuliaji na makipa kila mmoja akitoa mtazamo wake wakidai ni mwepesi na unapaa sana.
Mpira huo maalumu ulizunduliwa na kutambulishwa Septemba 22 jijini Dar es Salaam umeifanya Ligi Kuu Bara kuwa na utambulisho kama zilivyo ligi kubwa duniani zikiwemo Ligi Kuu ya England (EPL), La Liga, Serie A na Bundesliga, huku Afrika pia utaratibu huo ukiwa unatumika kwenye ligi kuu ya Afrika Kusini na Morocco ambazo zote hutumia mipira maalumu iliyoundwa kwa ubora wa hali ya juu na ambayo hutolewa mapema ili wachezaji na timu kuuzoea kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Hata hivyo, licha ya juhudi hizo na historia hiyo kubwa kwa soka la Tanzania, baadhi ya wachezaji na makocha mbalimbali wa timu za Ligi Kuu Bara wamekuwa na mitizamo tofauti kuhusiana na mpira huo, jambo linaloibua gumzo kutokana na ubora ulionao.
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, alisema mpira unaotumika kwa sasa hauko katika viwango walivyozoea, kwa sababu unaweza ukaupiga sehemu uliyokusudia ila ukaenda kwingine, hivyo, kama kunawezekana ufanyiwe maboresho ya haraka sana kabla ya mambo hayaharibika mbele ya safari.
Kauli hiyo iliungwa na kocha wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi, aliyesema mpira unaotumika kwa sasa una shida, ikiwa ni muda mfupi tangu timu hiyo ishinde bao 1-0 dhidi ya maafande wa Mashujaa, katika pambano lililopigwa, Septemba 30, 2025.
Kipa wa Namungo raia wa Burundi, Jonathan Nahimana alisema mpira wa sasa unazidiwa ubora mkubwa na uliotumika kwa msimu uliopita, kwa sababu huu wa sasa una ujazo mkubwa na hata ukipiga sehemu uliyokusudia ni ngumu kwenda kama unavyotaka.
“Mpira wa sasa hivi tunaotumia unayumba sana kwa maana hautulii mguuni, kwa mfano mechi yetu na Simba kuna muda naupiga ili ukamfikie mchezaji fulani, ila kwa bahati mbaya unapoteza pia mwelekeo na kwenda sehemu nyingine,” alisema kipa huyo wa kimataifa wa Burundi.
Mshambuliaji wa Coastal Union, Athumani Masumbuko ‘Makambo’, alisema bila kuonyesha juhudi binafsi ni ngumu kuweza kuutumia mpira huo wa sasa hivi, kwa sababu hautulii mguuni na unapocheza viwanja visivyoboreshwa inakuwa changamoto zaidi.
“Siyo siri kuna changamoto juu ya huu mpira, kwani usipokuwa makini unaweza kuonekana unazingua wakati kinachosababisha ni aina ya mpira, hatutapata nafasi ya kuutumia mapema mazoezini ili kuuzoea, wahusika walifanyie kazi haraka,” alisema Masumbuko anayemiliki bao moja kwa sasa.
Kwa upande wa kipa wa Mashujaa, Patrick Munthary, alisema mpira wa sasa ni mwepesi na unapoteza mwelekeo tofauti na wa msimu uliopita.
Wachezaji wengine ambao hawakutaka kutajwa majina yao, baadhi walikiri hawaoni tofauti yoyote ya mpira huo na wa misimu ya nyuma, ingawa wanashangaa kuzinduliwa na kutambulishwa wakati timu zimeshaanza kucheza ligi na hawana mazoezini.
“Ninavyojua mpira mpira unatakiwa kusambazwa mapema hata kabla ligi haijaanza ili wachezaji wauzoee, ila kwetu tumekutana nao uwanjani, hii sio sawa na ndio maana tunashindwa kuutumia,” alisema mmoja ya nyota hao, huku mwingine akisema hakuwa anajua kama mpira unaotumika ni mpya.
Mmoja wa mabosi wa klabu ya ligi hiyo kutoka mkoani, alisema bado hawajapewa mpira kama inavyotakiwa, lakini wanakutana nao uwanjani na kuhoji labda kwa timu za Dar es Salaam ndizo zilizofikiriwa kwani hata mazoezini wanaonekana kuwa nayo.
Mwananchi lilimtafuta Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB), Ibrahim Mwayela ili atoe ufafanuzi juu ya madai hayo ya mpira huo mpya wa Ligi Kuu, lakini alisema atafutwe Ofisa Habari wa bodi hiyo, Karim Boimanda.
Boimanda alipopatikana alisema hadi wakati anahojiwa mchana hawakuwa wamepata malalamiko juu ya mpira huo, lakini watalifanyia kazi kwa haraka kana kuna tatizo lolote.
“Hatujapata hayo madai kwa sasa. Ila Bodi itakusanya maelezo ya walioutumia mpira huo kisha itatoa taarifa rasmi kwa umma,” alisema Boimanda.
Hata hivyo, Ligi Kuu Bara siyo ya kwanza kwa makocha na wachezaji kulalamikia mipira kwani msimu uliopita kocha wa Arsenal Mikel Arteta aliulalamikia hadharani mpira uliokuwa ukitumika kwenye Kombe la Carabao.
“Mpira ni mbovu, unapepea sana, siyo mzuri ni vyema mamlaka zikatazama vizuri aina ya mipira kwenye ligi hizi.”
Mwanzoni mwa mwaka huu, kocha wa Man City Pep Guardiola, naye alitoa malalamiko yake kuhusu mipira inayotumika kwenye ligi za chini nchini England akisema haina ubora kama inayotumika Ligi Kuu, pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pep alisema hayo baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 kwenye Kombe la FA dhidi ya Plymouth huku akisema ni ajabu timu yake kupiga mashuti 20 na yote yanatoka nje.
“Mpira unaotumika kwenye Ligi Kuu Premier uko sawa, Ligi ya Mabingwa Ulaya sawa, lakini huu wa makombe mengine England hapana, hauna ubora hata kidogo.
“Ukipoteza mchezo unaonekana unalalamika, lakini ukweli ni kwamba mpira huu hauna ubora wa kutumika alisema Pep moja ya makocha wakubwa duniani.
Mbali na hivyo, pia wachezaji wengi waliulalamikia mpira uliotumika kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 ‘Jabulan’ ambao makipa wengi walisema kuwa ulikuwa unateleza mikononi, huku wafungaji wakisema kuwa ulikuwa mwepesi kupita kiasi.
SIFA ZA MPIRA
Licha ya kulalamikiwa, mpira huo uliotambulishwa rasmi Septemba 22, 2025, siku tano tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu 2025-2026, umetajwa na ubora wa kimataifa ambapo vipengele vilivyowekwa wakati wa utambulisho vinasomeka hivi;
Vipengele vya Mpira
– Ni moja kati ya mipira bora ya kitaalamu iliyotengenezwa kwa ubora wa hali ya juu na muonekano wa kuvutia.
– Imetengenezwa kwa ngozi maalum ya sintetiki rafiki kwa mazingira, pamoja na tabaka 4 za kitambaa maalum na safu ya ndani ya TPU, ikileta mpira wenye ubora mzuri na mguso laini.
– Una vipande 32 vilivyoshonwa kwa mkono, vinavyohakikisha mpira unaenda sawasawa na kuwa thabiti hata baada ya makumi ya maelfu ya mateke.
– Teknolojia ya High Frequency Embossing inaboresha urahisi wa kuuchezea na muonekano wa mpira.
– Ndani yake kuna blada ya mpira laini yenye valve ya ubora wa juu kuzuia upotevu wa hewa.
– Haunyonyi maji kwa urahisi kwa sababu ya mbinu maalum ya kushona paneli, hivyo unaweza kuutumia hata katika mvua bila matatizo.
– Huu ni mpira wa kiwango cha juu cha FIFA QUALITY PRO.