Bi. Ukpoma-Olaiya akitoa mifano ya baadhi ya miradi ambayo UNCDF imeitekeleza barani Afrika anasema Rwanda ni mfano bora ambapo UNCDF ilishirikiana na taasisi ya kifedha ya ndani kutoa dhamana na mtaji nafuu kusaidia biashara za kilimo zinazomilikiwa na vijana na wanawake. Aidha, UNCDF imewezesha upatikanaji wa fedha kwa vituo vidogo vya afya vijijini Rwanda, hatua iliyosaidia jamii kupata huduma bora za matibabu licha ya changamoto ya mtaji.
“Cha kipekee kuhusu hili ni kwamba UNCDF ilifanya kazi kupitia taasisi ya kifedha ya ndani ili kupunguza hatari kwenye uwekezaji huu na kuhakikisha kuwa mtaji unasambaa. Sasa tuligundua pia kwamba kuna hamasa ndani ya taasisi ya kifedha ya ndani, lakini kwa sababu ya uwezekano wa kiwango kikubwa cha hasara, mtaji haukusambaa. Kwa hivyo UNCDF iliingilia kati, ikawekeza kupitia dhamana kwa taasisi ya kifedha ya ndani, jambo lililoruhusu taasisi ya kifedha kutoa mtaji kwa biashara za kilimo.” Anasema.

Omon Ukpoma-Olaiya Kiongozi wa Timu ya Uwekezaji ya Kanda ya UNCDF kwa Afrika Mashariki na Kusini na Mataifa ya Kiarabu akihojiwa na Anold Kayanda huko New York, Marekani (Sept 2025)
Burundi
Huko Burundi, UNCDF ilishirikiana na Benki ya Wanawake Burundi, taasisi inayomilikiwa na serikali, kufanikisha upatikanaji wa mtaji kwa biashara zinazomilikiwa na wanawake. Hatua hii imefungua fursa za kifedha kwa wajasiriamali wanawake na kuongeza ushiriki wao katika kukuza uchumi.
Malawi
Katika Malawi, UNCDF iliwekeza katika shirika la ndani la ZUWETO, likitoa mtaji wa kufanya biashara ambao uliwawezesha kukuza shughuli zao za kilimo na kupata ufadhili zaidi kutoka masoko ya mitaji. Kwa sasa, ZUWETO imepata ufadhili wa ufuatiliaji ili kupanua biashara zao katika vifaa vya kutotolesha vifaranga na dawa za mifugo.
Anafafanua akisema, “tulifanikiwa kufanya upatikanaji wa fedha kwa shirika la Kimalawi linaloitwa ZUWETO. Mwanzoni tulitoa mtaji wa kufanya biashara kwa ZUWETO ili kuwawezesha kukuza biashara zao za kilimo. Baada ya mtaji huu wa kichocheo kutoka UNCDF, ZUWETO iliweza kupata ufadhili zaidi kupitia masoko ya mitaji. Sasa, hatukuishia hapo kwa sababu tumepata idhini ya kutoa ufadhili wa ufuatiliaji kwa ZUWETO ili kuwawezesha kupanua biashara yao, hasa kwenye vifaa vya kutotolesha vifaranga, kuongeza upatikanaji wa dawa za mifugo na bidhaa nyingine.”
Zimbabwe
Akimalizia, Bi. Ukpoma-Olaiya anataja mafanikio makubwa Zimbabwe, nchi ambayo takribani asilimia 46 ya watu hukosa umeme, hasa vijijini. Kupitia ushirikiano na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa pamoja, UNCDF imewezesha kuanzishwa kwa mfuko wa kwanza wa nishati mbadala. Hii imefanikisha miradi ya nishati ya jua ikiwemo hospitali, kiwanda cha kusindika maziwa cha Dairibord na Hospitali ya Mater Dei.
Kwa mujibu wa Bi. Ukpoma-Olaiya, miradi hii ni ushahidi wa jinsi ya kupunguza hatari za kifedha na kufungua fursa za uwekezaji zinazowalenga vijana, wanawake na jamii za vijijini barani Afrika.