
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzya, amesema kuwa hatua ya baadhi ya mataifa ya Magharibi kurejesha vikwazo kupitia utaratibu wa “snapback” dhidi ya Iran haina msingi wa kisheria na inakiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Nebenzya ametoa kauli hiyo kupitia barua ndefu aliyoituma kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama, baada ya baraza hilo lenye wanachama 15 kupiga kura ya kurejesha vikwazo vilivyofutwa chini ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani, yakiwemo Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, yanayojulikana kama troika ya Ulaya (E3).
Balozi huyo wa Russia amesisitiza kuwa utaratibu huo wa “snapback” ulianzishwa licha ya juhudi za kidiplomasia zilizofanyika kwa nguvu katika wiki mbili zilizopita, na licha ya Iran kuonyesha utayari wa kushiriki katika kutafuta suluhisho. Amesema mataifa ya E3 yalikataa maridhiano yote na kuchagua njia ya kuchochea mvutano.
Nebenzya ameongeza kuwa: “Madai ya E3 kuwa utaratibu wa ‘snapback’ umeanzishwa hayana mashiko yoyote, kwani mataifa hayo hayakufuata taratibu za utatuzi wa migogoro zilizowekwa na Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), ambao ni sehemu ya azimio namba 2231.” Ameongeza kuwa: “Zaidi ya hayo, ukiukaji mwingi wa nyaraka hizo uliofanywa na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani uliwanyang’anya haki ya kutumia kifungu hicho. Hivyo basi, ‘taarifa’ yao ya kuanzisha vikwazo kwa kutumia mfumo wa ‘snapback’ haina uhalali wa kisheria.”
Ameongeza kuwa: “Azimio lililowasilishwa katika Baraza la Usalama tarehe 19 Septemba halikutimiza masharti ya azimio 2231, na matokeo ya mjadala wake hayawezi kuhalalisha kurejeshwa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran. Kwa msingi huo, utaratibu wa ‘snapback’ hauwezi kuchukuliwa kuwa umeanzishwa.”
Balozi huyo wa Russia amesema kuwa kwa kuwa Baraza la Usalama halikupitisha azimio la kiufundi la kuongeza muda wa azimio 2231, basi litakoma kutumika kufikia tarehe ya mwisho ya JCPOA mnamo Oktoba 18, 2025. Baada ya hapo, masharti na kanuni zote, ikiwemo zile zinazohusu mpango wa nyuklia wa Iran, zitapoteza umuhimu wake.
Mgogoro kuhusu utaratibu wa “snapback” ulianza tangu makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 maarufu kama JCPOA, ambapo Iran ilikubali masharti ya kuaminika kuhusu mpango wake wa nyuklia kwa ajili ya kuondolewa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa, Marekani, na Umoja wa Ulaya.
Iran imesisitiza kuwa hatua yake ya kupunguza utekelezaji wa baadhi ya ahadi chini ya makubaliano ya JCPOA ilikuwa ya kisheria na halali, ikijibu kushindwa kwa Marekani na Umoja wa Ulaya kutimiza majukumu yao. Kwa msingi huo, mataifa ya E3 (Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani) hayana nafasi ya kuanzisha tena utaratibu wa vikwazo.
Russia, China, na baadhi ya mataifa mengine yameunga mkono msimamo wa Iran, yakitangaza kuwa hayatatambua kurejeshwa kwa vikwazo dhidi ya Tehran. Mataifa haya yanasisitiza kuwa hatua hiyo ya kurejesha vikwazo ni kinyume cha sheria za kimataifa na inakiuka azimio la Umoja wa Mataifa namba 2231.