“Baada ya zaidi ya siku 500 za kuzingirwa bila kukoma na mapigano yasiyoisha, El Fasher iko kwenye ukingo wa janga kubwa zaidi ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa kulegeza mzingiro wa kijeshi kwenye mji huo na kuwalinda raia,” amesema Türk.

Taarifailiyotolewa Geneva, Uswisi leo na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, (OHCHR) imesema ripoti ya kwamba RSF imeweka ndege zisizo na rubani za masafa marefu huko Darfur Kusini zimezua wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa kuongezeka kwa mapigano katika siku zijazo.

Kamishna huyo amesema raia wanaendelea kubeba mzigo mzito wa mashambulizi ya kiholela na yaliyoelekezwa moja kwa moja, huku mapigano yakiongezeka El Fasher.

Mauaji ya raia yanaendelea

Kati ya tarehe 19 hadi 29 Septemba, takribani raia 91 waliuawa kutokana na mashambulizi ya mizinga, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani, na uvamizi wa ardhini.

Pamoja na mashambulizi ya mara kwa mara kwenye maeneo ya kiraia, hali hii inaashiria jaribio la kuwafurusha kwa nguvu raia kutoka El Fasher, wakiwemo wakimbizi wa ndani katika kambi ya Abu Shouk.

Wiki  iliyopita, mtaa wa Daraja Oula jijini humo, ambao umepokea raia waliokimbia kambi ya Abu Shouk, umeshambuliwa mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na mashambulizi mawili ya ndege zisizo na rubani katika soko, na shambulio la awali kwenye msikiti lililoua takribani raia 67.

OHCHR imepokea ripoti za kuaminika kwamba takribani raia 23 waliuawa baada ya jiko la kijamii kushambuliwa kwa mizinga katika mtaa wa Abu Shouk.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN amesisitiza haja ya dharura ya kuhakikisha ulinzi kwa raia waliobaki El Fasher, hasa wale wasioweza kuondoka, kama vile wazee, watu wenye ulemavu, na wale wenye maradhi sugu.

“Raia lazima wahakikishiwe usafiri salama na wa hiari kutoka El Fasher, na katika safari yao kwenye njia kuu za kutokea na kwenye vituo vya ukaguzi vinavyodhibitiwa na makundi tofauti ya kijeshi,” amesema Türk, kufuatia ripoti za mara kwa mara za ukatili mkubwa dhidi ya wakimbizi, ikiwemo mauaji ya bila hukumu, mateso, utekaji na uporaji.

Hatari dhidi ya raia

Amebainisha hatari ya kurejea kwa mifumo ya ukiukaji wa haki unaochochewa na misingi ya kikabila dhidi ya raia, kama ilivyoshuhudiwa wakati wa mashambulizi ya RSF kwenye kambi ya Zamzam mwezi Aprili, ambapo kuliripotiwa matumizi ya kingono ya kikatili dhidi ya wanawake na wasichana wa jamii ya Zaghawa.

Pia amezitaka pande zote katika mzozo kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia mjini humo mara moja bila vikwazo, kwani mahitaji ni ya dharura sana.

Wito wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN unakuja wakati wa kipindi kigumu sana kwa raia waliokwama El Fasher, ambao wana upatikanaji mdogo sana wa chakula, maji na huduma za afya.

Soma taarifa nzima hapa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *