Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, katika ripoti yake inaishtumu serikali ya Tanzania kwa kuminya uhuru wa kisiasa, hatua ambayo inatilia shaka iwapo uchaguzi mkuu wa tarehe 29 mwezi huu utakuwa wa huru na haki.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Human Rights Watch katika ripoti yake, inasema serikali nchini Tanzania, imeendelea kukandamiza wanasiasa wa upinzani na wakosoaji wa chama tawala CCM, kuminya uhuru wa vyombo vya Habari, na kuingilia uhuru wa Tume ya Uchaguzi.

Nomathamsanqa Masiko-Mpaka, mtafiti wa Shirika hilo barani Afrika, amesema serikali ya Tanzania, inapaswa kuacha vitendo hivyo na badala yake kushiriki kwenye majadiliano na wapinzani wake, ili kuleta mageuzi muhimu, yatakayosaidia uchaguzi huo kuwa huru na haki.

Aidha, Shirika hilo linasema, limenakili visa 10 ambapo wapinzani wa serikali, wametekwa, kukamatwa na kuteswa kwa sababu ya misimamo yao ya kisiasa, akiwemo kiongozi mkuu wa upinzani Tundu Lissu ambaye alikamatwa mwezi Aprili, na kufunguliwa mashtaka ya uhaini.

Wafuasi wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wa Chama tawala cha CCM wakihudhuria mkutano wa kampeni jijini Dar Es Salaam.
Wafuasi wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wa Chama tawala cha CCM wakihudhuria mkutano wa kampeni jijini Dar Es Salaam. REUTERS – Emmanuel Herman

Ripoti hiyo imetaja kisa cha kutekwa kwa mwanaharakati wa kisiasa kutoka chama cha upinzani CHADEMA, Mpaluka Nyagali, maarufu kama Mdude ambaye alitekwa nyumbani kwake huko Mbeya, na mpaka sasa hajukani alipo. Polisi wameendelea kusema hawahusiki na kutoweka kwake.

Human Rights Watch inasema,  iliaandikia serikali ya Tanzania, ikiwemo Wizara ya Mambo ya nje, barua kuomba majibu yao, kuhusu utafiti huu lakini hadi kuchapishwa kwa ripoti hii Septemba tarehe 30, haikupokea majibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *