Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha kikosi kikubwa zaidi cha usalama cha kimataifa kwa ajili ya Haiti kwa ajili ya kukabiliana na ghasia za magenge zinazoongezeka katika nchi hiyo yenye migogoro.

Kikosi hicho kinachojulikana kama “Gang Suppression Force” (GSF) kitakuwa na hadi polisi na wanajeshi 5,550 wenye uwezo wa kuwaweka kizuizini washukiwa wa magenge yanayoendesha ghasia.

GSF itaongeza ujumbe wa Kimataifa wa Msaada wa Usalama unaoongozwa na Kenya (MSS) – kikosi ambacho kilikusudiwa kuwa na hadi wanachama 2,500, lakini kikakumbwa na upungufu mkubwa na kimekuwa na wakati mgumu kuzuia ghasia tangu kutumwa nchini humo mwaka 2023. Zaidi ya watu 5,500 waliuawa katika ghasia zinazohusiana na magenge nchini Haiti mwaka wa 2024. Magenge yenye silaha kwa sasa yanadhibiti takriban 85% ya mji mkuu, Port-au-Prince.

Ingawa jiji kuu, Port-au-Prince, ndio kiini cha machafuko, vurugu zimeanza kuenea kwa kasi katika maeneo mengine ya nchi. Katika mikoa ya Centre na Artibonite, mashambulizi ya makundi yenye silaha yamewalazimisha makumi ya maelfu kuhama makazi yao. Idadi ya watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao ndani ya Haiti imefikia takriban milioni 1.3, ikiwa ni ongezeko la asilimia 24 tangu Desemba 2024, na sasa ndiyo idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa kutokana na machafuko nchini humo, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).

Ghasia za magenge zimeikumba Haiti kwa miaka mingi, lakini zimeongezeka zaidi tangu kuuawa Rais Jovenel Moise mnamo 2021.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *