Israel imesema itawarejesha walikotoka wanaharakati wa Ulaya,waliokuwa kwenye msafara wa kuwapelekea msaada Wapalestina wa Gaza.
Juhudi za wanaharakati hao zilikatizwa jana usiku pale boti zao zilipozuiwa na wanajeshi wa majini wa Israel katika bahari ya Mediterrania.
Jeshi la wanamaji la Israel lilizingira maboti kiasi 45 ya msaada yaliyokuwa na wanaharakati waliojizatiti kuwafikia Wapalestina wa Gaza wanaokabiliwa na madhila makubwa ya njaa, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kufuatia operesheni ya kijeshi inayofanywa na Israel kwenye eneo hilo.
Mzingiro wa jeshi la wanamaji la Israel pwani ya Gaza
Israel iliwaonya wanaharakati hao dhidi ya kuingia kwenye eneo la bahari ambalo imesema liko chini ya mzingiro.
Miongoni mwa meli zilizokamatwa na kuzuiwa ni pamoja na ile aliyokuwemo mwanaharakati maarufu duniani Greta Thunberg.
Kufikia hivi leo Alhamisi,ripoti za wanaofuatilia msafara huo wa Samud Flottila zinaonesha kati ya vyombo vya majini 45 vilivyokuwa njiani 30 vimekamatwa na kuzuiwa na Israel.
Kwenye taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Israel iliyochapisha kwenye mtandao wake wa X hivi leo, imeuita msafara huo ni Hamas Sumud na umefika salama na kwa amani katika pwani ya Israel ambako mchakato wa kuwarudisha Ulaya utaanza.
Taarifa hiyo imefafanuwa zaidi kwa kusema kwamba abiria wa msafara huo wako salama na kwenye afya nzuri na kuchapisha pia picha za wanahakarati akiwemo Greta Thunberg.
Waliopanga safari hiyo Sumud Flottila wametowa pia taarifa wakiiokosoa hatua ya Israel wakisema imekiuka sheria katika eneo la bahari la Kimataifa.
Ulimwengu walaani hatua ya Israel
Mamlaka ya Wapalestina kupitia msemaji wa wizara yake ya mambo ya nje nayo imelaani hatua ya Israel ikisema imevunja sheria ya kimataifa kwa kuingia kwa nguvu bila ridhaa yake katika maeneo ya bahari yake ikiwemo pwani ya Ukanda wa Gaza.
Uturuki, Colombia, Pakistan, Malaysia na Afrika Kusini ambayo raia wake, mjukuu wa mpigania Ukombozi, Nelson Mandela, ni miongoni mwa mataifa yaliyoikosoa Israel huku Uingereza ikisema imewasiliana na mamlaka za Israel kuhakikisha kwamba suala hili linatatuliwa kwa njia salama kwa kuzingatia sheria ya Kimataifa na haki za binadamu.
Hali ndani ya Gaza
Umoja wa Mataifa umesema hautoondowa wafanyakazi wake au ofisi zake Gaza City licha ya kuongezeka hatari kufuatia kuanza upya kwa operesheni za kijeshi za Israel.
“Mamlaka za Israel zinafahamu wazi wajibu wao wa kulinda Majengo ya Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wake na wanafahamu hasa wapi tunakofanyakazi. Tunawashirikisha kuhusu nyendo zetu. Na nafikiri takriban kila siku tunajadili kuhusu kinachokwenda sawa sawa na kisichokwenda sawa. Wenzetu wa usalama wanachukulia kazi yao kwa umaniki mkubwa. Tunajaribu kukwepa na kupunguza hatari katika mazingira ya kutisha. Lakini kufikia sasa tunaendelea kuwepo Gaza City”
Tamko la Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric la kuthibitisha msimamo wa Umoja wa Mataifa wa kuendelea kutoa msaada wa kibinadamu Gaza umetolewa jana Jumatano baada ya waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz kuonya kwamba watu watakaoeendelea kubakia Gaza City watachukuliwa kama magaidi na waungaji mkono ugaidi.