Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya Watanzania kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mijadala ya kisiasa imezidi kushika kasi nchini.
Wananchi katika maeneo mbalimbali wameanza kueleza wazi kuchoshwa na utawala wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakilalamikia changamoto za huduma za kijamii.
Huduma duni za maji, afya, ajira na usafiri zimetajwa mara kwa mara kama sababu kuu zinazowafanya wananchi kutangaza kutoridhishwa kwao na chama tawala.
Katika baadhi ya masoko na foleni za maji, wananchi walisikika wakilalamika kwa sauti moja: “Hali ni ngumu, huduma hazitufikii, sasa hivi CCM tumechoka.”
Kauli hizi zimezua mijadala iwapo mwelekeo huu unaweza kuwa ishara ya mabadiliko makubwa katika siasa za Tanzania.
Vurugu na taharuki kabla ya uchaguzi
Moja ya matukio yaliyosisimua hisia ni vurugu katika kituo cha mabasi ya mwendokasi Magomeni jijini Dar es Salaam.
Wananchi waliandamana, wakapiga mawe na kuvunja baadhi ya mabasi wakipinga huduma zisizoridhisha na wakisema hawakitaki tena CCM.
Mmoja wao alisikika akisema: “Sio kwamba tunapinga maendeleo, lakini tunataka kuona vitendo, sio maneno tu.”
Mara baada ya vurugu hizo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliwataka wananchi kupunguza jazba.
“Watanzania wa Dar es Salaam waendelee kuvumilia kidogo, mabasi yanakuja. Hata ukisema huitaki CCM, humtaki Mama haisaidii,” alisema Chalamila.
Wachambuzi waonya kuhusu mabadiliko
Wachambuzi wa siasa wanasema matukio haya ni ujumbe mzito kwa vyama vyote, hasa chama tawala, kwamba wananchi wanahitaji mabadiliko ya kweli.
Profesa Aboubakar Kinyondo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema kila changamoto ya kijamii imekuwa ikitumiwa na wananchi kuonyesha msimamo wao wa kisiasa.
“Kila mara inapojitokeza changamoto ya kijamii, wananchi wanatumia nafasi hiyo kutoa msimamo wao wa kisiasa,” alisema Prof. Kinyondo.
Kwa mtazamo wake, hii ni ishara kwamba sauti ya wananchi inataka kusikika zaidi kuliko miaka ya nyuma, na inaleta changamoto mpya kwa viongozi.
Kadri siku ya uchaguzi inavyokaribia, swali kubwa linasalia: je, sauti hizi za wananchi zitatafsiriwa vipi kwenye matokeo ya sanduku la kura?