Watu wawili wameuawa na wengine watatu kujeruhiwa vibaya baada ya shambulizi la gari na kisu lililotokea nje ya sinagogi kaskazini magharibi mwa Manchester, Uingereza. Shambulizi hilo lililotajwa na polisi kama la kigaidi lilitokea wakati wa sikukuu takatifu ya Kiyahudi ya Yom Kippur, na limeibua taharuki kubwa katika jamii ya Wayahudi nchini humo.
Polisi wa Manchester (GMP) walisema mshukiwa mmoja mwanaume alipigwa risasi na kuuawa na maafisa waliokuwa na silaha, baada ya jaribio la kumkamata kushindikana. Ripoti za awali zilionyesha hofu kwamba mshukiwa alikuwa na bomu lililofungwa mwilini, na kikosi cha kutegua mabomu kilitumwa eneo la tukio. Baadaye polisi walithibitisha hakuna kitisho cha milipuko kilichobakia.
Polisi walieleza kuwa idadi kubwa ya waumini walikuwa ndani ya sinagogi la Heaton Park wakati wa shambulizi, na wote waliamriwa kuondoka kwa tahadhari. Polisi pia walisema watu watatu waliojeruhiwa wako katika hali mahututi na wanapokea matibabu hospitalini.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, aliyekuwa Copenhagen kwenye mkutano wa viongozi wa Ulaya, alikatisha ziara yake na kurejea haraka London kushughulikia kitisho hiki cha usalama. Starmer alisema ameshtushwa na shambulio hilo na mawazo yake yako kwa wale wote walioathirika.
Alitangaza kuongoza kikao cha dharura cha kamati ya usalama wa taifa, COBRA, na kuongeza kuwa vifaa na nyenzo za ziada vya polisi vinatumwa kwa masinagogi kote nchini. “Tutafanya kila kitu kuiweka jamii ya Kiyahudi salama,” alisema Starmer, akibainisha pia kuwa ukweli kwamba shambulio limefanywa siku ya Yom Kippur unalifanya kuwa la kutisha zaidi.
Tahadhari na mwitikio wa dharura
Meya wa Manchester Andy Burnham pamoja na taasisi ya usalama wa jamii ya Wayahudi (CST) walipongezwa kwa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama. Serikali imesema juhudi za haraka za vikosi vya dharura zimeokoa maisha na kupunguza hofu kwa jamii.
Katika eneo la Crumpsall karibu na Manchester, sauti kubwa ya mlipuko ilisikika wakati kikosi cha kutegua mabomu kilipoingia ndani ya gari la mshambuliaji kwa tahadhari.
Mashuhuda walisema walihisi kama kulikuwa na mlipuko mkubwa, ingawa polisi walieleza kuwa hiyo ilikuwa sehemu ya operesheni ya kudhibiti vifaa vilivyokuwa ndani ya gari.
Baadaye walithibitisha hakuna kitisho cha milipuko na wakaazi walihimizwa kurejea katika hali ya kawaida.
Mfalme Charles III na Malkia Camilla walitoa salamu za rambirambi, wakisema wameshtushwa na kuhuzunishwa sana na shambulio hilo, hasa likitokea siku muhimu ya kidini. Walisema mawazo yao yako kwa familia zilizopoteza wapendwa na kwa jamii ya Kiyahudi kwa ujumla.
Polisi wa London nao walitangaza kuimarisha ulinzi kwa kutuma maafisa wa ziada kupiga doria katika maeneo yanayozunguka masinagogi na vituo vya jamii ya Kiyahudi, ingawa walibainisha hakuna dalili ya kitisho kipya katika jiji hilo.
Serikali ya Uingereza imeweka wazi kuwa shambulio hili litaangaliwa kama kipaumbele cha kitaifa la kiusalama. Starmer amesema serikali yake haitavumilia vitisho vya aina hii na itaongeza msaada wa kiusalama katika maeneo yote yenye hatari kubwa.
Hofu ya ugaidi na mshikamano wa jamii
Wataalamu wa usalama wameonya kuwa mashambulizi dhidi ya maeneo ya kidini ni changamoto kubwa inayohitaji mshikamano wa kijamii na ushirikiano wa karibu wa vikosi vya usalama. Wamesema uhalifu huu ni jaribio la kuchochea hofu na mgawanyiko wa kijamii.
Kwa sasa uchunguzi wa kina unaendelea, huku umma ukihimizwa kuwa macho, kushirikiana na polisi na kuepuka kusambaza uvumi. Manchester na Uingereza kwa ujumla zimeachwa zikijitafakari juu ya namna bora ya kulinda raia wake bila kupoteza mshikamano wa kijamii na imani kwa vyombo vya usalama.