Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amewaonya viongozi wa Ulaya kwamba mashambulizi ya karibuni ya ndege zisizo na rubani yanaonyesha Russia inataka kuongeza moto wa vita.

Akizungumza katika mkutano wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya mjini Copenhagen, Zelensky alisema hatua hiyo ni tishio linalovuka mipaka ya Ukraine.

“Ndege zisizo na rubani zilizoonekana kote Ulaya ni ishara kuwa Russia bado inajiona imara vya kutosha kuongeza vita hivi,” alisema Zelensky.

Aliongeza kuwa mashambulizi hayo siyo juu ya Ukraine pekee, bali ni mkakati wa Moscow wa kuivunja Ulaya na Magharibi kwa ujumla.

Viongozi wa karibu mataifa 50 wanakutana mjini Copenhagen chini ya ulinzi mkali, kufuatia mashaka yaliyosababishwa na kuingia kwa droni zinazoshukiwa kuwa za Urusi katika anga za Denmark, Estonia na Poland.

Denmark Copenhagen 2025 | Volodymyr Zelensky akizungumza na Edi Rama, Friedrich Merz na Keir Starmer katika mkutano wa kilele wa EPC
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akizungumza na Waziri Mkuu wa Albania Edi Rama, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na Waziri Mkuu wa Uingereza Kier Starmer siku ya mkutano wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya mjini Copenhagen, Denmark, Oktoba 2, 2025.Picha: Mads Claus Rasmussen/Ritzau Scanpix/REUTERS

Ulaya yajipanga kwa ukuta wa droni

Viongozi wa Ulaya wameonyesha nia ya kushirikiana na Ukraine kujifunza uzoefu wake wa vita ili kuimarisha ulinzi wao.

Mpango unaojadiliwa ni kujenga “ukuta wa droni” ili kuzuia mashambulizi yanayoweza kufanywa na Moscow.

Zelensky alionya kwamba kama Russia inaweza kutuma droni Poland au nchi za kaskazini mwa Ulaya, basi hakuna taifa lililo salama.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alisisitiza kuwa ni muhimu kuwa na msimamo thabiti dhidi ya mashambulizi hayo.

“Droni zitakazokiuka mipaka yetu zinaweka hatari kubwa, na zinaweza kuharibiwa mara moja,” alisema Macron.

Shinikizo jipya dhidi ya Russia

Waziri Mkuu wa Romania, Nicosur Dan, alionya kuwa jeshi lake litapiga chini droni yoyote ya Russia itakayovuka anga la nchi yake tena.

Macron pia alitoa wito wa kuzidisha shinikizo dhidi ya “shadow fleet,” meli kongwe zinazotumika kusafirisha mafuta ya Russia kinyume cha vikwazo.

Denmark Copenhagen 2025 | Mette Frederiksen, Volodymyr Zelensky na Antonio Costa wakiwa kwenye mkutano wa kilele wa EPC
Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa wakipiga soga wakati wa picha ya pamoja katika mkutano wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya mjini Copenhagen, Denmark, Oktoba 2, 2025.Picha: Leonhard Foeger/REUTERS

Alisema hatua ya kuzima biashara hiyo ni muhimu kwa kuwa itapunguza uwezo wa Moscow kufadhili vita vyake.

Wakati huohuo, Umoja wa Ulaya unajadili pendekezo la kutumia mali zilizozuwiwa za Russia kufadhili mkopo mpya wa euro bilioni 140 kwa Ukraine.

Belgium, ambako mali nyingi zimehifadhiwa, bado ina wasiwasi mkubwa na inataka dhamana kwamba hatari itagawanywa na mataifa yote ya Umoja wa Ulaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *