Mara baada ya taarifa za kifo chake kutangazwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia Naibu  msemaji wake Farhan Haq ameelezea masikitisho yake kwa kifo cha Jane Goodall na amemshukuru kwa juhudi zake za za kulinda mazingira na kwa msaada wake mkubwa kwa Umoja wa Mataifa.

Amesema “akiwa Mjumbe wa Amani wa Umoja wa Mataifa kwa zaidi ya miongo miwili, sauti ya Dkt. Goodall iliiletea dunia uelewa mkubwa juu ya umuhimu wa kulinda mazingira yetu. Mchango wake utaendelea kuongoza na kuhamasisha juhudi za pamoja za binadamu kwa ajili ya amani, maendeleo endelevu, na uwiano na asili.”

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, UNEP kupitia mtandao wa X, limesema Dkt. Goodall atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa uhifadhi na mazingira.

Programu yake ya Roots and Shoots iliyosambaa duniani kote imesaidia makumi ya maelfu ya vijana katika takribani nchi 100 kuendesha miradi ya kusaidia binadamu. Wanyama na mazingira.

Tarehe 10 mwezi Aprili mwaka 2002 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Kofi Annan Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo alimtangaza Goodall kuwa mjumbe wa amani.

Annan kupitia mshereheshaji wa hafla hiyo alisema, ” Kwa kutambua kwamba katika kipindi chote cha taaluma yako ya kipekee kama mwanasayansi wa tabianchi na mtetezi wa mazingira, umeonesha kujitolea kwako kwa kile kilicho bora zaidi kwa ubinadamu; tukiwa na ufahamu kwamba mfano wako umeonesha kile kinachoweza kufikiwa pale watu wenye nia njema wanapoungana kwa ajili ya dunia bora; na tukiwa na matumaini kwamba kupitia mchango wako katika maendeleo endelevu, ujumbe wa amani, maelewano na heshima utasikika kote duniani – ninajivunia na nina furaha kubwa kumtangaza Jane Goodall kuwa Mjumbe wa Amani.”

Mwenyewe Bi. Goodall baada ya kupewa heshima hiyo ya kuwa mjumbe wa amani, akasema, “Kila mmoja wetu ana mchango fulani katika sayari kila siku tunayoishi, na tuko katika nafasi ya kipekee ya kuweza kuchagua aina ya athari tunayotaka kuleta. Sisi ni sehemu ya aina ya ajabu ya wanyama, na tutafikia uwezo wetu wa kweli kama wanadamu pale akili na moyo vitakapofanya kazi kwa maelewano.”

Alianzisha pia taasisi ya Jane Goodall inayotambuliwa kote duniani kwa programu za ubunifu wa mbinu za uhifadhi barani Afrika, ambako alianza masomo yake mwaka 1960.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *