Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) leo limezindua rasmi mpira utakaotumika katika Fainali za Kombe la Dunia 2026 ambazo zitafanyika katika nchi za Mexico, Canada na Marekani.
Mpira huo unajulikana kwa jina la Adidas Trionda likimaanisha mawimbi matatu.
Baada ya kuzinduliwa rasmi, mpira huo tayari umeshaanza kuuzwa kwa bei ya Dola 160 (Sh392800) kwa kila mmoja.

Mpira huo ndani yake umewekewa teknolojia ya akili mnemba kwa ajili ya kuwasaidia wachezaji na marefa kutokana na teknolojia hiyo kuwa na uwezo wa kujulisha matukio ya kuotea na kushika mpira kwa mkono.
Ni mpira wenye rangi nne ambazo ni nyeupe iliyochukua nafasi kubwa, nyekundu, bluu na kijani ambazo ni rangi za mataifa matatu yanayoandaa fainali hizo za Kombe la Dunia.
Kwa mujibu wa FIFA, mpira huo wa Adidas Trionda ni ukumbusho wa Mpira wa Brazuca ambao ulitumika katika Fainali za Kombe la Dunia 2014 zilizofanyika Brazi.

“Ni mpira unaoonekana zaidi wa Kombe la Dunia la FIFA ambao tumewahi kuunda. Ni kitu cha ufundi kilichojengwa kwa ajili ya jukwaa kubwa zaidi, ambacho hukufanya utake kuushikilia, kuushangaa, na zaidi ya yote k’ucheza nao.
“Mfumo wa chipu umewekwa ndani, ukiwa na wimbi la kisasa zaidi la Teknolojia ya Mpira Uliounganishwa ya Adidas, ambayo hupeleka data kwenye mfumo wa VAR,” amesema Sam Handy, meneja mkuu wa Adidas Football.

Nyota wa Real Madrid, Jude Belllingham, staa wa Inter Miami, Lionel Messi na nyota wa Barcelona, Lamine Yamal wameoneka katika picha mbalimbali wakiushika na kuuchezea mpira huo.