
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imelaani vikali mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya msafara wa kimataifa wa meli nyingi wa Sumud ukielekea Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa yake jana Alkhamisi, Hamas imetaja uchokozi huo dhidi ya msafara wa meli, wanaharakati, na waandishi wa habari kama “shambulio la hila, jinai ya uharamia na ugaidi wa baharini.”
“Tunalaani vikali uchokozi wa kikatili ulioanzishwa na adui dhidi ya ‘Sumud Flotilla’ na tunathibitisha kwamba kuzizuia meli hizo ni kitendo cha uhalifu ambacho kinapaswa kulaaniwa na watu wote walio huru duniani,” imeongeza taarifa ya Hamas.
Kundi hilo la Muqawama hata hivyo, limepongeza ujasiri na azma ya wanaharakati hao ya kuvunja mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza ambao umeharibiwa na vita vya mauaji ya halaiki vya Israel.
Kadhalika imetoa wito wa kufanyika harakati za maandamano ya kimataifa kwa ajili ya kulaani uchokozi huo wa Wazayuni, na kukemea duniani kote ukatili huo.
Tayari maandamano makubwa yameshuhudiwa katika nchi za Ulaya kupinga mashambulizi hayo ya utawala wa Israel dhidi ya msafara wa kimataifa wa Sumud. Kwa mujibu wa ripoti, maandamano yamefanyika nchini Italia, Ubelgiji, Ujerumani, Ufaransa, Ugiriki, Uturuki na nchi nyingine za Ulaya.
Boti nyingi za msafara wa kimaataifa wa meli zipatazo 50 unaojulikana kama (Sumud) zilivamiwa Jumatano na jeshi la wanamaji la Israel zilipokuwa zikikaribia Ukanda wa Gaza, ambapo wanaharakati kadhaa walijeruhuwa, huku wengine wakizuiliwa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali kitendo hicho cha utawala ghasibu wa Israel cha kuvamia kijeshi msafara huo wa kimataifa, na kueleza kuwa ukatili uliofanywa na Israel unadhihirisha ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kukitaja kitendo hicho kuwa ni ugaidi.